IQNA

Uingereza yatakiwa kufafanua maana ya 'Chuki Dhidi ya Uislamu' (Islamophobia)

16:21 - October 23, 2025
Habari ID: 3481402
IQNA- Kufuatia ongezeko kubwa la uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza, serikali inatarajiwa kutangaza ufafanuzi mpya wa neno “'Chuki Dhidi ya Uislamu' (Islamophobia)”—ambapo huenda likabadilishwa na kuwa “chuki dhidi ya Waislamu.”

Jopo huru lililoongozwa na waziri wa zamani wa chama cha Conservative, Dominic Grieve, limekuwa likichunguza suala hili tangu Februari, likilenga kufafanua vitendo visivyokubalika vya ubaguzi, chuki, na dhulma dhidi ya Waislamu au wale wanaoonekana kuwa Waislamu.

Lord Khan, mwanachama wa chama cha Labour na waziri wa zamani wa masuala ya imani, ambaye alianzisha mchakato huu, ametoa wito kwa serikali kuidhinisha kikamilifu tafsiri hiyo mpya bila kuipunguza. Amesisitiza kuwa tafsiri hiyo inapaswa kuakisi hali halisi ya maisha ya Waislamu wa Uingereza na kufuata malengo ya awali ya uchunguzi huo. Khan alieleza kuwa huu ni wakati wa kushughulikia tatizo sugu katika jamii, akibainisha kuwa yeye binafsi ni miongoni mwa waliokumbwa na chuki hiyo.

Serikali imeeleza kuwa tafsiri yoyote mpya haitakiwi kukandamiza uhuru wa kujieleza. Maafisa wamesisitiza kuwa haki ya kukosoa au kutokubaliana na imani za kidini lazima ilindwe, na kwamba tafsiri hiyo haipaswi kufungua mlango wa sheria za kukataza kukufuru.

Mnamo mwaka wa 2021, chama cha Labour kilikubali tafsiri inayosema kuwa 'Islamophobia' ina mizizi ya ubaguzi wa rangi na inalenga taswira zima ya Uislamu. Tafsiri hii ya awali imekumbwa na ukosoaji kutoka kwa wabunge wa Conservative, akiwemo Claire Coutinho, aliyeeleza kuwa kutoa ulinzi maalum kwa kundi moja kunaweza kuchochea chuki zaidi. Alilinganisha tafsiri hiyo na ile ya chuki dhidi ya Wayahudi, ambayo ilikubalika kimataifa kwa sababu ilikabiliana na suala mahsusi—kukanusha mauaji ya Holocaust.

Waislamu wa Uingereza wanasema bado wanakumbwa na ubaguzi, na bila tafsiri rasmi ya 'Islamophobia', uhalifu mwingi huenda usiripotiwe. Takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonesha ongezeko la 20% la uhalifu wa chuki za kidini mwaka uliopita, ambapo karibu nusu ya waathiriwa walikuwa Waislamu.

Hata hivyo, baadhi ya taasisi za sera zinaonya kuwa kuidhinisha tafsiri hiyo kunaweza kuathiri sheria za kupambana na ugaidi na kudhoofisha mpango wa Prevent. Uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutangazwa na Waziri wa Jumuiya, Steve Reed, huku serikali ikisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza utaendelea kulindwa.

Muhtasari wa Makala ya Serena Barker-Singh

3495118

Habari zinazohusiana
captcha