Katika hafla ya heshima iliyofanyika siku ya Jumatatu, bendera hiyo nyeusi iliinuliwa kwa ishara ya maombolezo. Tukio hilo lilihudhuriwa na wahudumu wa Haram au kaburi tukufu, mawakili wa haram, wafanyaziara, na wakaazi wa eneo hilo waliokusanyika kwa unyenyekevu kumuenzi Bi Fatima (SA) — anayehesabiwa katika Uislamu kuwa mfano wa uchamungu, huruma, na msimamo dhidi ya dhulma.
Wakati wa hafla hiyo, pazia nyeusi juu ya dharih (eneo takatifu la kaburi) pia lilibadilishwa, kuashiria mwanzo wa siku za maombolezo katika eneo hilo tukufu.
Ibada maalum za maombolezo, usomaji wa Qur’ani, na khutba zimeratibiwa kwa muda wa wiki nzima ili kuenzi urithi wake wa kiroho.
Kaburi la Imam Ridha (AS) lililoko Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran, ni miongoni mwa vituo muhimu vya Ziyara za kidini katika ulimwengu wa Kiislamu. Ndani yake ndimo yalipo mapumziko ya Imam Ali ibn Musa al-Ridha (AS), Imam wa nane wa Kishia, na huvutia mamilioni ya wafanyaziyara kila mwaka. Eneo hilo pia linajumuisha viwanja vikubwa, maktaba, vyuo vya dini, na makumbusho , likihudumu kama kitovu cha kiroho na kitamaduni.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele.
Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo mwa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali bin Abi Talib AS na Waisalmu wengine waliosabilia nafsi zao kwa ajili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na alilea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (SAW) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi.
Wanazuoni wamezungumzia mengi kuhusu utukufu wa Hadhrat Fatima (AS) na wamemtaja kama mfano kamili wa mwanamke Mwislamu. Kwa sababu hiyo, Mtume Muhammad (SAW) alimtaja Bibi Fatima (S) kinara wa wanawake wa dunia.
Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchamungu na elimu kubwa na alikuwa mfano na kigezo chema cha Waislamu.
Hafla za maombolezo katika haram hiyo zitaendelea katika siku zijazo, kwa mikusanyiko ya waumini na wasomaji wa Qur’ani wakimuenzi Bi Fatima (SA) na sifa zake tukufu.