IQNA

Kozi ya Mafunzo kwa Majaji wa Mashindano ya Qur’an Yafanyika Nchini Algeria

17:07 - November 03, 2025
Habari ID: 3481457
IQNA – Waziri wa Awqaf wa Algeria, Youssef Belmahdi, ametangaza kukamilika kwa kozi ya tatu ya mafunzo kwa majaji wa mashindano ya Qur’ani Tukufu nchini humo.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 71 ya Mapinduzi ya Algeria yaliyofanyika jijini Algiers, Belmahdi alisema kuwa kozi hiyo iliwahusisha majaji 17 wa kiume na wa kike, pamoja na zaidi ya washiriki 70 waliotoka miongoni mwa maimamu na wahubiri au walinganizi wa Kiislamu kutoka mikoa mbalimbali.

Waziri huyo alieleza pia maendeleo ya hali ya juu yaliyopatikana katika nyanja ya mafunzo ya uamuzi wa mashindano ya Qur’ani Tukufu, kutokana na programu zilizoratibiwa na Taasisi ya Kisasa ya Usomaji wa Qur’ani kwa njia ya mtandao (Virtual Recitation Institute) na Kituo cha Kielektroniki cha Usomaji wa Qur’ani cha Algeria.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Belmahdi alisisitiza kuwa wanazuoni wa Algeria wamekuwa wakibeba ujumbe wa nuru na elimu katika historia, na wamekuwa na mchango mkubwa katika kueneza maarifa na mamlaka ya kidini barani Afrika na Ulaya.

Aliongeza kuwa kabla ya ukoloni, Algeria ilikuwa ni kitovu cha elimu na wanazuoni waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha taasisi mashuhuri kama Al-Zaytouna, Al-Azhar, pamoja na taasisi za Maka, Madina, na maeneo ya Sham.

Algeria ni nchi ya Afrika Kaskazini ambapo Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia tisini na tisa ya idadi ya watu.

3495239

Kishikizo: algeria qurani tukufu
captcha