IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi: Mzozo wa Iran na Marekani ni wa dhati

7:06 - November 04, 2025
Habari ID: 3481461
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema kuwa mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani ni wa “dhati na wa kweli”, na wala hautokani na kauli mbiu; bali unatokana na mgongano wa kimsingi wa maslahi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema kuwa mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani ni wa “dhati na wa kweli”, na wala hautokani na kauli mbiu; bali unatokana na mgongano wa kimsingi wa maslahi.

Amesema suala la ushirikiano na Marekani linaweza kufikiriwa katika siku za usoni, lakini si sasa wala katika kipindi cha karibu, isipokuwa pale tu Washington itakapositisha kikamilifu utoaji wa msukumo, misaada na uungaji mkono kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, iache kuingilia masuala ya Iran, na iondoe kambi zake za kijeshi katika eneo hili.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo Jumatatu jijini Tehran alipohutubia maelfu ya wanafunzi, wanachuo na familia za mashahidi wa Vita vya Siku 12, kwa mnasaba wa tarehe 4 Novemba, siku ya kuadhimisha Siku ya Wanafunzi na Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani, ambayo inasadifiana na kumbukumbu ya kutekwa kwa “Pango la Ujasusi”, yaani ubalozi wa zamani wa Marekani mjini Tehran mwaka 1979. Amesisitiza kuwa tukio hilo ni la kihistoria na linaonesha utambulisho halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa: “Mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani ni wa dhati halisi na ni mgongano wa maslahi kati ya pande mbili. Ni ikiwa tu Marekani itakomesha kikamilifu uungaji mkono wake kwa utawala uliolaaniwa wa Kizayuni, ikaondoa kambi zake za kijeshi katika eneo, na ikaacha kuingilia masuala ya Iran; ndipo ombi la Marekani la ushirikiano na Iran litazingatiwa , na si sasa wala katika siku za karibuni, bali huko mbeleni.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema pia kuwa kutekwa kwa ubalozi wa Marekani mwaka 1979 ni “siku ya fahari na ushindi” na kielelezo cha utambulisho halisi wa serikali ya Marekani.

Amebaini kwamba: “Kutekwa kwa ubalozi wa Marekani kulifichua utambulisho halisi wa serikali ya Marekani na dhati ya Mapinduzi ya Kiislamu.”

Ayatullah Khamenei ameeleza kwamba chimbuko la mivutano kati ya Marekani na Iran linarejea kwenye mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1953 yaliyompindua Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh. Amesema Marekani, kwa kushirikiana na Uingereza, ilipanga njama dhidi ya Mossadegh licha ya kujionyesha hadharani kuwa inamuunga mkono.

Amesema: “Wamarekani walionyesha tabasamu kwa Mossadegh, lakini kisirisiri, wakiwa na Waingereza, wakaandaa mapinduzi ya kijeshi, wakaipindua serikali ya kitaifa, na kumrudisha Shah aliyekuwa ametoroka.”

Aidha, Ayatullah Khamenei amejibu madai kwamba kauli mbiu kama “Mauti kwa Marekani” ndizo zinazochochea uadui wa Washington dhidi ya Iran. Ameongeza kuwa: “Suala la Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ni la dhati, ni mgongano wa maslahi, si kauli mbiu.”

Pia amekumbusha kuwa tukio la kutekwa kwa ubalozi wa Marekani mwaka 1979 lilitarajiwa kudumu kwa siku chache kama nembo ya kuonyesha hasira ya umma, lakini baadaye lilifichua njama kubwa zilizokuwa zimepangwa dhidi ya Mapinduzi.

Amesema: “Wanachuo waligundua nyaraka zilizoonyesha kuwa ubalozi huo ulikuwa kitovu cha njama dhidi ya Mapinduzi.”

Katika hotuba hiyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahimiza wanafunzi kuongeza maarifa na uelewa kuhusu historia ya kisiasa ya Iran na changamoto za sasa, kuimarisha sayansi, na kuendeleza uwezo wa kijeshi ili kuonyesha kwamba “Iran ni taifa imara, ambalo hakuna dola linaloweza kulitiiisha au kulipigisha magoti.”

4314495

Habari zinazohusiana
captcha