IQNA

16:07 - November 08, 2019
News ID: 3472206
TEHRAN (IQNA) -Rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza kuwa mafaili ya ufisadi wa kifedha yatafikishwa katika mahakama za nchi hiyo kwa ajili ya uchunguzi.

Akizungumza Alhamisi alisema maandamano ya wananchi wa Lebanon yamepelekea viongozi wa nchi hiyo kutangaza vita dhidi ya mafisadi ambao aghalabu ni wanasiasa wa sasa na wa zamani.

Alisema baadhi ya viongozi au wanasiasa wa sasa na wa zamani wa Lebanon ambao ni washukiwa wa ufisadi wa kifedha wataanza kusailiwa bila kujali nyadhifa zao. Aidha alisema kuwa, serikali ijayo ya Lebanon itaundwa na mawaziri wanaostahiki na ambao hawakabiliwi na tuhuma za ufisadi.

Kuanzia 17 Oktoba Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi. Ingawa Saad Al Hariri amejiuzulu kama waziri mkuu wa Lebanon, lakini maandamano ya wananchi yangali yanaendelea. Moja ya sababu kuu za maandamano ya watu wa Lebanon ni ufisadi mkubwa nchini humo hasa ufisadi wa kifedha.

Lebanon inakumbwa na matatizo makubwa ya kisiasa ikiwa ni pamoja na deni la dola bilioni 86, ukosefu wa ajira ambao kiwango chake kinakaribia asilimia 35 miongoni mwa vijana na kuongezeka umasikini nchini humo.

Iwapo wakuu wa Lebanon wataweza kukabiliana na ufisadi ipasavyo basi wataweza kurejesha imani ya wananchi iliyotoweka na kwa msingi huo kuandaa mazingira ya kuwepo serikali yenye kutenda kazi kwa maslahi ya taifa.

Nukta nyingine muhimu ya kutatua mgogoro wa sasa na vita dhidi ya ufisadi Lebanon ni kuwa hakupaswi kuwa  na uingilaji wa ajinabi katika maambo ya ndani ya nchi hiyo hasa katika kuundwa serikali.

3855251

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: