IQNA

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel atakiwa kuomba radhi kwa kuunga mkono Ufasisti wa Chuki Dhidi ya Waislamu

19:19 - October 11, 2025
Habari ID: 3481353
IQNA – Mwanasiasa kutoka Venezuela, Bi Maria Corina Machado, ambaye ametunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2025, ametakiwa kuomba msamaha na kujitenga na misimamo yake ya kuunga mkono ufasisti unaoeneza chuki dhidi ya Waislamu.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), ambalo ndilo shirika kubwa zaidi la kutetea haki za Waislamu nchini humo, limelaani vikali uamuzi wa kamati ya Nobel kumpa Machado tuzo hiyo, likiuita “wa kudhalilisha na usiokubalika.”

CAIR limesema kuwa kuchagua kumheshimu Machado – mwanasiasa anayejulikana kwa kuunga mkono harakati za siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya na chama tawala cha Likud la utawala dhalimu wa Israel – ni dharau kwa wale waliopigania haki dhidi ya ubaguzi wa rangi, ufasisti, na mauaji ya halaiki yanayoendelea huko Gaza.

“Tuzo ya Amani ya Nobel inapaswa kutolewa kwa wale walioonyesha msimamo wa kimaadili kwa kutetea haki kwa watu wote kwa ujasiri, si kwa wanasiasa wanaodai demokrasia kwao huku wakiunga mkono ubaguzi, chuki, na ufasisti nje ya nchi yao,” CAIR ilisema kupitia taarifa kutoka makao yake makuu mjini Washington, D.C.

CAIR imemtaka Machado kuomba msamaha na kujitenga na kauli zake za awali pamoja na ushiriki wake katika mkutano wa Patriots of Europe uliofanyika Madrid mapema mwaka huu, ambapo wanasiasa kama Geert Wilders, Marine Le Pen, na Viktor Orban walitoa wito wa kufukuzwa kwa Waislamu Ulaya.

“Tunamwomba Bi Machado ajitenge na chama cha Likud na misimamo ya ufasisti wa chuki dhidi ya Waislamu barani Ulaya,” CAIR ilisema. “Akikataa, basi kamati ya Nobel inapaswa kufikiria upya uamuzi wake, ambao umeharibu heshima ya tuzo hiyo. Mtu mwenye chuki dhidi ya Waislamu na muungaji mkono wa ufasisti wa Ulaya hastahili kutajwa sambamba na watu kama Dkt. Martin Luther King Jr. na washindi wengine wa heshima hiyo.”

CAIR ilisema kamati ya Nobel inapaswa badala yake kuwaheshimu “wanafunzi, waandishi wa habari, wanaharakati, au wahudumu wa afya walioweka maisha yao hatarini kupinga mauaji ya halaiki huko Gaza” – watu ambao, kwa mujibu wa shirika hilo, ndio wanaoakisi roho halisi ya amani na haki.

Mnamo mwezi Februari, Machado alitoa hotuba ya mtandaoni katika mkutano wa Patriots of Europe, ambapo viongozi wa siasa kali walikashifu uhamiaji na kusifu kufukuzwa kwa Waislamu kutoka Iberia katika enzi za kati. Kwa mujibu wa Reuters, ujumbe wa video wa Machado ndio uliufungua mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa siasa kali kutoka Ulaya nzima.

Machado pia ameonyesha kuunga mkono serikali ya mrengo wa kulia ya Israel. Mnamo mwaka 2020, alitia saini makubaliano rasmi ya ushirikiano kati ya chama chake cha siasa na chama cha Likud, na baadaye akatangaza, “Mapambano ya Venezuela ni mapambano ya Israel.” Ameahidi kuhamisha ubalozi wa Venezuela hadi Jerusalem al-Quds, akidhihirisha kuunga mkono uvamizi haramu wa mji huo na utawala wa Israel.

CAIR ilihitimisha kwa kusema kuwa kumheshimu mtu kama huyo “ni kudhalilisha urithi wa Tuzo ya Amani ya Nobel” na kupuuza mateso ya waathirika wa vita na dhulma duniani kote.

3494957

Habari zinazohusiana
captcha