IQNA

13:29 - March 27, 2020
News ID: 3472606
TEHRAN (IQNA) - Idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 au corona nchini Marekani imeongezeka na kufikia watu 82,400, hiki kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi cha maambukizi ya ugonjwa huo hatari duniani hivi sasa.

Hayo ni kwa mujibu wa data zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins ambazo zinaonyesha kuwa, idadi hiyo ya maambukizi nchini Marekani imeipita ile ya China iliyokuwa ikiongoza kwa kesi  81,700, ikifuatiwa na Italia yenye 80,500 hadi kufikia sasa.

Hata hivyo Italia inaogoza kwa idadi ya vifo vya wagonjwa wa COVID-19 duniani, ambapo kufikia sasa walioaga dunia kutokana na ugonjwa huo katika nchi hiyo ya Ulaya ni watu 8,200.

Wakati huohuo, kufungwa kwa shughuli za kiuchumi kutokana na janga la corona nchini Marekani kumesababisha ongezeko kubwa la watu wanaosajiliwa kwenye orodha ya wasio na ajira na kufikia watu milioni 3.3, idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.

 

Karibu kila jimbo la Marekani limeyataja maradhi ya COVID-19 kama sababu kuu ya kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na kazi nchini humo.

Mbali na kupanda kwa kasi ya kutisha idadi ya watu walioambukizwa virusi vya COVID-19 nchini Marekani, lakini pia idadi ya vifo vya wagonjwa wa virusi hivyo imepindukia 1,000 kufikia sasa.

Kwa mujibu wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, hadi sasa kesi za maambukizi ya virusi vya corona kote duniani ni zaidi ya nusu milioni ambapo zaidi ya wagonjwa 23,000 wa COVID-19 wameaga duniani, huku wengine 120,000 wakipata nafuu baada ya kuambukizwa ugonjwa huo.

3470992

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: