IQNA

12:33 - March 24, 2020
News ID: 3472597
TEHRAN (IQNA) – Uongjwa wa COVID-19 maarufu kama corona umewaathiri Waislamu kote duniani hasa kutokana na kufungwa misikiti kwa muda ili kuzuia kuenea ugonjwa huo na hivi sasa viongozi wa Kiislamu wanabadilisha mbinu za kuwaongoza Waislamu kiroho.

Nchini Saudi Arabia,  msikiti Mtakatifu wa Makka (al-Masjid al-Ḥaram) na Msikiti Mtakatifu wa Mtume SAW (Al Masjid an Nabawi) imefungwa kwa muda usiojulikana kutokana na hofu ya kuenea kirusi cha corona.

Huko Kuwait,  sehemu ya adhana isemayo Hayya Aalas-Salah yaani njooni katika Sala  imeondolewa na badala yake Muadhini anasema  'al-salatu fi buyutikum' yaani Salaini katika majumba yenu. Hivi sasa maimamu wengi wanatoa hotuba ambazo zinarushwa moja kwa moja kupitia mitandao ya intaneti.

Imam Omar Suleiman wa Dallas, Texas nchini Marekani anasema kwa mara ya kwanza ametoa hotuba ya Sala ya Ijumaa moja kwa moja kupitia intaneti akiwa nyumbani.

Imam Suleiman anasema  hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja au mubashara kupitia intaneti haikulenga kuchukua mahala pa Sala ya Ijumaa bali ni njia ya kuwapa ushauri wa kiroho au kimaanawi wale walio nyumbani kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19.

Mapema mwezi huu, aghalabu ya misikiti Marekani ilianza kufungwa kwa muda kufuatia ushauri wakuu wa masuala ya afya ya umma kuhusu kufungwa maeneo yenye mijimuiko mikubwa kama vile misikiti, makanisa na viwanja vya michezo ili kuzuia kuenea ugonjwa wa corona.

Jumuiya ya Waislamu Marekani ambayo inaleta pamoja  vituo 50 vya Kiislamu kote Marekani imeunda jukwaa maalumu la intaneti linalotumiwa na maimamu na wanazuoni maarufu nchini humo kwa lengo la kutoa mawaidha, kusoma Qurani na pia kwa ajili ya Duaa.

Hadi sasa watu zaidi ya 46,000 wameambukizwa corona nchini Marekani huku watu  413 wakiwa wamefariki hadi sasa na hali imetabiriwa kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni.

3470978

 

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: