Kwa mujibu wa taarifa, idadi ya waliofariki na ugonjwa wa corona Marekani imepindukia 45,000 huku nchi hiyo inayojinadi kuwa dola lenye nguvu zaidi duniani ikionekana sasa kuhitajia misaada ya dharura kukabiliana na ugonjwa huo.
Misri tayari imeshatangaza kuwa inatuma Marekani ndege iliyosheheni vifaa na zana za kitiba za kukabiliana na virusi vya Corona.
Serikali ya Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ambayo imekuwa ikifanya jitihada za kuwa na uhusiano mzuri na utawala wa Rais Donald Trump ilituma ndege hiyo iliyobeba misaada ya kitiba nchini Marekani jana Jumanne. Barakoa au maski 200 000 ni sehemu ya msaada huo.
Mwanasiasa Dutch Ruppersberger ambaye anaongoza kundi la wabunge wa Bunge la Wawakilishi la Marekani kutetea uhusiano wa nchi hiyo na Misri amesema ndege hiyo ya misaada kutoka Misri imetua katika uwanja wa kijeshi wa Dutch Ruppersberger, nje kidogo ya mji mkuu Washington.
Kwa mujibu wa takwimu za leo za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini humo imefikia 819,000 huku zaidi ya 45,000 miongoni mwao wakifariki dunia kwa virusi hivyo.
Kwa sasa Marekani inashika nafasi ya kwanza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya corona na vilevile kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wahanga wa virusi hivyo.
Utawala wa Rais Donald Trump unalaumiwa kwa kuchukua hatua za kupima virusi vya vya corona kwa kuchelewa, na kutokana na kuwa na idadi kubwa ya malaki ya waathirika wa virusi hivyo, sasa nchi hiyo inasumbuliwa na uhaba wa vifaa na zana za kitiba za kukabiliana na janga hilo. Awali utawala wa Trump ulionekana kupuuza ukubwa wa janga la corona kabla ya kuchukua hatua baada ya idadi ya vifo kuongezeka. Aidha taarifa zinasema idadi kubwa ya wanaofariki kutokana na corona nchini Marekani ni Wamarekani wenye asili ya Afrika.
3471227