IQNA

Kiongozi Muadhamu katika ujumbe wa Siku ya Kimataifa ya Quds

Wigo wa Jihadi katika ardhi za Palestina upanuliwe

15:43 - May 22, 2020
Habari ID: 3472791
TEHRAN (IQNA) - Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito wa kupanuliwa wigo wa jihadi katika ardhi za Palestina.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran wakati alipozungumza kwa njia ya televisheni Ijumaa adhuhuri kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds.

Kiongozi Muadhamu ameashiria ukubwa wa maafa ya kughusubiwa nchi ya Palestina na kubuniwa kwa donda la saratani la uzayuni na kusisitiza kwamba mhalifu mkuu wa maafa ya Palestina ni serikali za nchi za Magharibi na siasa zao za kishetani.

Kiongozi Muuadhamu amesema, leo mrengo wa muqawama na mapambano unaendelea kuimarika kila siku kinyume na mrengo wa dhulma, kufr, na uistikbari ambao unaendelea kudhoofika na kukata tamaa. Amesema jambo hilo linathibitishwa wazi na ukweli kwamba hii leo jeshi la utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel ambalo wakati mmoja lilichukuliwa kuwa ni jeshi lisiloshindwa katika eneo la Asia Magharibi hii leo linapigishwa makoti na kudhalilishwa na wapiganaji wa makundi ya wananchi na Kiislamu katika nchi za Lebanon Ukanda wa Gaza na kulazimishwa kuondoka katika ulizozikalia kwa mabavu.

Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu alibainisha ukweli huo kuhusu kuangamia utawala wa Kizayuni sambamba na kuwasilisha uchambuzi kamili kuhusu matukio ya eneo ambapo amewasilisha nasaha saba muhimu kuhusu kuendelea jihadi kubwa na takatifu ya hivi sasa.

Nasaha hizo saba muhimu za Ayatullah Khamenei katika hotuba yake ya Siku ya Kimatiafa ya Quds ni pamoja na: “Kutoifanya kadhia ya Palestina kuwa kadhia ya Wapalestina au Waarabu tu”, “kukombolewa ardhi zote za Palestina kutoka bahari hadi mto na kurejea Wapalestina  wote katika ardhi zao”, “kujizuia kuyaamini madola makubwa ya kidhalimu ya Magharibi, taasisi tegemezi ya kimataifa na baadhi ya dola vibaraka katika eneo,” “vijana wenye ghera katika ulimwengu wa Kiislamu wafuatilie matakwa ya kukabiliana na njama za Wamarekani na Wazayuni”, “kukabiliana na hali mbaya na yenye madhara ya uwepo wa Wamarekani na Wazayuni”, “kuendeleza mapambano na kupanua wigo wa Jihadi katika ardhi za Palestina” na  “kufanyika kura ya maoni yenye kuwajumuisha Wapalestina wa  dini na kaumu zote.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria kuwa, “msimu mpya katika kupigania ukombozi wa Palestina ulianza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 na leo, kwa hima ya irada ya mrengo wa muqawama au mapambano,  tunashuhudia kubadilika mlingano wa nguvu kwa maslahi ya wanamapambano.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema natija ya kujisalimsha huku ni kupotosha mkondo wa mapambano na kuupeleka katika mazungumzo yasiyo na faida na Wazayuni  maghasibu na waungaji mkono wao. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: “Ni katika mazingra kama hayo ndio yakadhihiri Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na hivyo msimu mpya ukaanza katika mapambano ya Palestina. Baada ya kujitokeza mrengo wa muqawama na mapambano,  hali ya utawala wa Kizayuni imekuwa ngumu na bila shaka hali itazidi kuwa ngumu zaidi katika mustakabali.”

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nasaha zake akasisitiza kuwa, Palestina ni ya Wapalestina wote na inapaswa kusimamiwa kwa irada yao.  Kiongozi Muadhamu kwa mara nyingine amewasilisha mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kufanyika kura ya maoni yenye kuwahusisha Wapalestina wa dini na kaumu zote na kusema: “Mpango huu unaonyesha kuwa, madai ya chuki dhidi ya Uyahudi, ambayo yanakaririwa katika vyombo vya habari vya Kimagharibi hayana msingi wowote.”

Katika hotuba yake ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Kiongozi Muadhamu aliashiria pia ukweli mwingine na kusema: “Kile ambacho bila  shaka lazima kiangamie ni mfumo wa Kizayuni na Uzayuni.”

3900728

 

captcha