IQNA

Jumuiya ya Mwamko wa Kiislamu yapongeza Uturuki kwa kufungua Msikiti wa Hagia Sophia

16:27 - July 26, 2020
Habari ID: 3473000
TEHRAN (IQNA) – Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu imeipongeza Uturuki kwa hatua yake ya kulirejeshea jengo la kihistoria la Hagia Sophia hadi yake ya msikiti.

Katika taarifa, Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu imeitaja hatua hiyo ya Uturuki kuwa ya kishujaa na yenye kustahiki pongezi.

Jumuiya hiyo imelaani uharibifu uliotekelezwa dhidi ya maeneo ya Waislamu na ustaarabu wa Kiislamu katika vita vya msalaba na kuongeza kuwa, wakati Waislamu walipoteka maeneo ya ustaarabu wa Magharibi, hawakuyaharibi bali waliyageuza kuwa maeneo yao ya ibada na hivyo kuchangia katika maingiliano ya kiutamaduni.

Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu, yenye makao yake Tehran, Iran,  imetoa wito kwa Waislamu kuunga mkono hatua ya busara ya serikali ya Uturuki ya kugeuza Hagia Sophia kuwa msikiti na kusema hatua hiyo imelenga kuhuisha utambulisho wa Kiislamu na kuwarejeshea Waislamu turathi zao.

Sala ya kwanza ya Ijumaa ilisaliwa Ijumaa katika msitiki wa Hagia Sophia nchini Uturuki tarehe 24 mwezi huu wa Saba baada ya miaka 86 kwa kuhudhuriwa na rais, viongozi wa serikali na pia wananchi wa nchi hiyo.

Kufanyika Sala ya kwanza ya Ijumaa katika msikiti wa Hagia Sophia kuna umuhimu mkubwa kwa serikali na wananchi wa Uturuki na pia kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Ukweli ni kuwa hatua hiyo ya serikali ya Uturuki inaweza kutajwa kuwa ni ushindi mbele ya sehemu muhimu ya Ulimwengu wa Magharibi. Hasa ikizingatiwa kuwa, Marekani, aghalabu ya serikali za Magharibi na hata taasisi za kimataifa zilionyesha radiamali hasi kufuatia hatua ya Rais wa Uturuki ya kutangaza mwezi Mei mwaka huu suala la kubadili matumizi ya jumba hilo la makumbusho na kuwa msikiti wa Hagia Sophia.

Swala hiyo ya Ijumaa imefanyika wiki mbili baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kwamba, jengo hilo lenye umri wa karibu miaka 1,500 litafunguliwa kwa ajili ya ibada ya Waislamu kufuatia uamuzi wa ya Mahakama Kuu wa kubadilishaji matumizi ya jengo hilo lililofanywa jumba la makumbusho na mwanzilishi wa Uturuki ya sasa mwanzoni mwa miaka ya 1930.

Jumba la Hagia Sophia ni miongoni mwa maeneo yaliyowekwa kwenye orodha ya turathi za duni na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, na ni mojawapo ya vivutio vikuu vya watalii huko Istanbul.

3912640

captcha