IQNA

Iran yazitaka Armenia na Azerbaijan zijiepushe na mapigano

18:45 - September 28, 2020
Habari ID: 3473210
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka nchi za Armenia na Azerbaijan zijizuie na zisitishe mapigano yanayoshuhudiwa katika mpaka wa nchi mbili hizo tokea jana Jumapili.

Muhammad Javad Zarif ametoa mwito huo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Armenia, Zohrab Mnatsakanyan na wa Jamhuri ya  Azerbaijan, Jeyhun Bayramov ambapo amesisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi mbili hizo jirani kutochukua hatua zitakazoendelea kuwasha moto wa vita na taharuki.

Dakta Zarif ameziasa nchi mbili hizo kuanzisha mazungumzo haraka iwezekanavyo, katika fremu ya sheria za kimataifa.

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh sambamba na kuzitaka Armenia na Azerbaijan kusitisha vita na uhasama, amesema nchi hii iko tayari kuzipatanisha pande mbili hizo juu ya mgogoro wa eneo la Nagorno-Karabakh.

Mapigano baina ya majeshi ya nchi mbili hizo yalianza jana asubuhi na yameripotiwa kuendelea usiku kucha. Kwa mujibu wa televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, watu zaidi ya 30 wameuawa katika mapigano hayo ambayo yanashuhudiwa hadi sasa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Azerbaijan imesema leo Jumatatu kuwa, raia sita wa nchi hiyo ni miongoni mwa watu waliouawa katika mapigano hayo, huku wengine 19 wakijeruhiwa. Wakati huohuo, Vardan Toganyan, Balozi wa Armenia nchini Russia amesema askari 30 wa Armenia wameuawa, huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa katika vita hivyo.

Tangu mwaka 1991, nchi hizo mbili zimekuwa zikipigania jimbo la Nagorno-Karabakh lililojitangazia uhuru wake baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Eneo hilo liko katika ardhi ya Azerbaijan lakini linaedeshwa na watu wa makabila ya Armenia.

3925813

Kishikizo: iran armenia azerbaijan
captcha