IQNA

Adhana kwa mara ya kwanza mjini Shusha, Jamhuri ya Azerbaijan baada ya miaka 28 + Video

13:43 - November 12, 2020
Habari ID: 3473354
TEHRAN (IQNA) – Sauti ya adhana imesikika baada ya miaka 28 katika msikiti wa kihistoria Yukhari Govhar Agha katika mji wa Shusha ulioko eneo linalozozaniwa baina ya Jamhuri ya Azeribajan na Armenia la Nagorno-Karabakh.

Adhana imeweza kusikika katika mji wa Shusha baada ya jeshi la Jamhuri ya Azerbaijan kuukomboa kutoka mikononi mwa jeshi la Armenia. Mji huo ni wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh.

Klipu iliyosambaa katika mitandao ya kijamii imemuonyesha mwanajeshi wa Jamhuri ya Azerbaijan akiadhini katika msikiti huo wa kihistoria wa Yukhari Govhar Agha.

Mji wa shusha ulikaliwa kwa mabavu na wanajeshi wa Armenia mnamo Mei 8, 1992 na una umuhimu mkubwa wa kijeshi.

Hatua ya Jamhuri ya Azerbaijan kuukomboa mji huo ni ushindi mkubwa kwa nchi hiyo kabla ya mapatano ya usitishwaji vita ambayo yametiwa siani Novemba 19. Waislamu wa Shusha wamefurahi sana kusikia adhana mjini humo baada ya miongo mitatu ya ardhi hiyo kukaliwa kwa mabavu na nchi ya Kikristo ya Armenia.

Ingawa eneo la Nagorno-Karabakh ni la Jamhuri ya Azerbaijan kwa mujibu wa sheria za kimataifa lakini limekuwa likikaliwa kwa mabavu na nchi jirani ya Armenia.

Russia tangu Jumanne ilianza kupeleka wanajeshi wake 2000 wa kulinda amani katika eneo hilo la Nargono Karabakh baada ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan kufikia makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya wiki kadhaa katika jimbo hilo wanalolizozania.

Makubaliano hayo yaliibua shangwe nchini Jamhuri ya Azerbaijan lakini hayakufurahiwa nchini Armenia ambako waandamanaji waliingia mitaani kuwashutumu na kuwalaani viongozi wao kwa kulipoteza jimbo hilo lililojitenga na Jamhuri ya Azerbaijan katika vita vilivyoshuhudiwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 na kupelekea watu karibu 30,000 kupoteza maisha.

Chini ya mkataba huo, Jamhuri ya Azerbaijan itayadhibiti maeneo yote iliyoyakamata, ukiwemo mji wa pili kwa ukubwa wa mkoa huo, Shusha, nao wanajeshi wa Armenia wasalimishe udhibiti wa maeneo mengine kadhaa kati ya sasa na Desemba mosi.

3934783/

captcha