IQNA

Mohammad Bin Salman ametembea Israel mara kadhaa kwa siri

11:02 - October 07, 2020
Habari ID: 3473237
TEHRAN (IQNA) – Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammad bin Salman, ameutembelea utawala wa Kizayuni wa Israel mara kadhaa kwa siri, amefichua afisa wa zamani wa usalama katika utawala huo.

"Mohammad bin Salman amefurahia jua la Tel Aviv mara kadhaa," amesema afisa huyo wa zamani wa shirika la Israel la usalama wa ndani, Shin Bet, wakati akizungumza na Televisheni ya Al Mayadeen ya Lebanon kwa sharti kuwa jina lake lisitajwe.

Hii si mara ya kwanza kwa safari za Bin Salman Israel kufichuka. Mnamo Oktoba 2017, afisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel alithibitisha kuwa Bin Salman amefika mara kadhaa Israel na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa utawala huo.

Safari hizo zinafanyika wakati ambao Saudi Arabia na Israel hazina uhusiano rasmi wa kidiplomasia. Hatahivyo kuna ripoti kadhaa kuwa Israel na Saudia zimekuwa zikikurubiana katika miaka ya hivi karibuni.

Saudia imekuwa ikiongoza mikakati ya nyuma ya pazia ya kutaka nchi za Kiarabu ziwe na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Tarehe 15 mwezi wa Septemba mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu katika ikulu ya rais wa Marekani, White House mjini Washington.  Hadi hivi sasa ulimwengu mzima wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu, kama Afrika Kusini zinalaani kitendo hicho cha kisaliti cha Bahrain na UAE. Hatua hiyo ya UAE na Bahrain imetajwa kuwa ni usaliti kwa kwa malengo ya ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

3472737

captcha