IQNA

10:47 - March 08, 2020
News ID: 3472545
TEHRAN (IQNA) - Askari wa Gadi ya Mfalme wa Saudi Arabia imetekeleza amri ya mrithi wa mfalme wa nchi hiyo, Mohammad bin Salman na kuwatia nguvuni wanamfalme watatu wa nchi hiyo kwa tuhuma za uhaini.

Ahmed bin Abdulaziz Al Saud, ndugu wa Mfalme Salman pamoja na mpwa wa mfalme huyo Muhammad bin Nayef  na vilevile Nawaf bin Nayef ambaye ni ndugu wa mrithi wa zamani wa ufalme wa Saudia, wametiwa nguvuni na askari wa Gadi ya Mfalme. Wanamfalme hao wanakabiliwa na tuhuma za kufanya uhaini huku kukiwa na tetesi kuwa hali ya Mfalme Salman bin Abdulaziz ni mahututi na anakaribia mauti. Kwa msingi huo Bin Salman ameanzisha mkakati wa kujitayarisha kutwaa madaraka kamili huku akiwakamata wale wote wanaoonekana kupinga mkakati wake huo.

Historia ya utawala wa Aal Saudi huko Hijaz inaonesha kwamba, kipindi cha utawala wa Mfalme Salman bin Abdulaziz na mwanaye, Muhammad ndicho kilichoshuhudia ukandamizaji na mashaka makubwa zaidi kwa wanamfalme wa Saudia au kwa uchache tunaweza kusema kuwa ni nadra sana kuweza kupata kipindi ambacho wanamfalme wa nchi hiyo walipata mashaka makubwa zaidi ya kipindi cha utawala wa sasa. Mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman ambaye anajitambua kuwa ndiye mfalme amekuwa akifuatilia kwa karibu sana harakati zote za wanamfalme wa nchi hiyo. Si hayo tu bali ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na nafasi na uwezo wa wanamfalme wenzake na kwa msingi huo amekuwa akitumia stratijia ya kuwatia nguvuni wanamfalme hao kama njia ya kuimarisha nafasi yake na kung'ang'ania kiti cha ufalme. 

Novemba mwaka 2017 wanawafalme na wanasiasa mashuhuri zaidi ya 200 wa Saudia walitiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini kwa amri ya Muhammad bin Salman kwa tuhuma za kufanya ufisadi, miongoni mwao alikuwemo bilionea mwanamfalme Al Waleed bin Talal, ambaye alishikiliwa kwenye hoteli ya Ritz Carlton. Imeripotiwa kuwa Bin Salman alipokea zaidi ya dola bilioni mia moja kwa watu hao kama kikomboleo cha kuwaachia huru. Baada ya kamatakata hiyo ya wanamfalme ilifuatia zamu ya kutiwa nguvuni wanazuoni wa Kiislamu, waandishi na wanaharakati wa Saudi Arabia.

Tunaweza kusema kuwa Muhammad bin Salman anaendesha kampeni hiyo na kuwakandamiza wanamfalme wenzake, wanazuoni na wanaharakati kwa shabaha ya kuimarisha satua na ushawishi wake katika madaraka ya nchi na vilevile kunyamazisha sauti zote za upinzani zinazomkosoa.

Kwa sasa Bin Salman amewasweka jela wapinzani wake wawili wakuu. Ahmed bin Abdulaziz ni miongoni mwa watoto wa mwasisi wa dola la Saudia, Abdulaziz al Saud na ndugu wa mfalme wa sasa wa nchi hiyo. Anatambuliwa na wanamfalme wengi wa Saudia kuwa ndiye anayestahiki kuwa mfalme wa Saudi Arabia baada ya Salman bin Abdulaziz. Ahmad bin Abdulaziz amekuwa akikosoa siasa zinazotekelezwa na Muhammad bin Salman.

Muhammad bin Nayef alikuwa mrithi wa ufalme wa Saudia kabla ya mfalme wa sasa, Salman bin Abdulaziz kumuondoa kwenye nafasi hiyo mwaka 2017 na kumteuwa mwanaye, Muhamma bin Salman kuchukua nafasi hiyo. Harakati hiyo ilitambuliwa na wachambuzi wa mambo kuwa ni “mapinduzi bubu” na ya kimyakimya. Hata hivyo Muhammad bin Nayef ameendelea kuwa na satua na ushawishi mkubwa katika utawala wa Saudi Arabia na anatambuliwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushika kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Muhammad bin Nayef amekuwa katika kifungo cha nyumbani tangu miaka mitatu iliyopita na hata picha zake hazionekani katika vyombo vya habari isipokuwa kwa nadra sana.

Japokuwa Ahmed bin Abdulaziz Al Saud na Muhammad bin Nayef wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kufanya uhaini lakini hapana shaka kuwa, hatua hiyo inatokana na woga wa Muhmmad bin Salman kutokana na tishio la wanamfalme wapinzani. Woga na wahka huo umekuwa mkubwa sana kwa kadiri kwamba, mkutano na hata mazungumzo ya aina yoyote ile kati ya wanamfalme yanatambuliwa na utawala kuwa ni “njama ya uhaini”.

3883816

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: