IQNA

RIPOTI

Netanyahu anapanga kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Bin Salman

8:08 - February 08, 2020
Habari ID: 3472449
TEHRAN (IQNA) – Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu anapanga kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman.

Kwa mujibu wa jarida ya Kiebrania la Israel Defense,  wakuu wa utawala wa Kizayuni wanataka kuhakikisha kuwa mkutano huo unafanyika katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, kabla ya uchaguzi wa bunge la Israel, uliopangwa kufanyika Machi 2.

Ripoti hiyo imesema mkutano huo utafanyika katika fremu ya mkakati wa utawala haramu wa Israel wa kuimarisha uhusiano na nchi za Kiarabu. Ripoti hiyo imedokeza kuwa mkutano baina ya Netanyahu na Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan, ambao ulifanyika hivi karibuni Entebbe, Uganda ulipangwa na Umoja wa Falme za Kiarabu. Mkutano huo umelaaniwa vikali nchini Sudan huku baraza la mawaziri likisema halikujulishwa.

Mwezi Aprili 2018, Gazeti la al Manar la Palestina lilichapisha ripoti iliyosema kuwa, mfalme wa Saudi Arabia ndiye muhandisi wa uhusiano wa Wasaudia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuandika kuwa: Tangu mwanzoni mwa mwaka 1990, mfalme wa hivi sasa wa Saudia ana uhusiano wa karibu na Israel.

Gazeti hilo la Palestina limezinukuu duru za kuaminika zikifichua kuwa: Mawasiliano ya siri na ya kificho baina ya Salman bin Abdulaziz Aal Saud, mfalme wa hivi sasa wa Saudi Arabia na Israel yamekuwepo tangu Salman alipokuwa amir wa Riyadh. Tangu wakati huo alikuwa na mawasiliano ya karibu na watu kama Is'haq Rabin, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ripoti ya gazeti hilo imesisitiza kuwa, Salman alimuunganisha mwanawe Muhammad bin Salman kwenye mawasiliano hayo maalumu na Israel tangu miaka kadhaa nyuma.

Juhudi za waziwazi za Saudia za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zinafanyika katika hali ambayo kwenye miaka ya hivi karibuni, mbali na Israel kuwakandamiza vibaya Wapalestina na kuendelea kuteka ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, inaendelea pia kuzikalia kwa mabavu ardhi nyingine za Kiarabu-Kiislamu hasa kibla cha kwanza cha Waislamu, yaani Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds.

3470561

 

captcha