IQNA

Wapalestina wamkosoa vikali balozi wa zamani wa Saudia nchini Marekani

20:17 - October 10, 2020
Habari ID: 3473247
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imemkosoa vikali balozi wa zamani wa Saudi Arabia nchini Marekani kutokana na matamshi yake dhidi ya wapigania ukombozi wa Palestina.

Katika taarifa HAMAS na PLO zimemlaani vikali mwanamfalme  Bandar bin Sultan bin Abdulaziz Al Saud, ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la Saudia na kusema matamshi yake ya hivi karibuni ni ya kusikitisha.

Bandar bin Sultan amewakosoa vikali viongozi wa Palestina kwa kupinga hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Katika mahojiano na Televisheni ya al-Arabiya ya Saudia, Bandar bin Sultan bin Abdulaziz amesema, kitendo hicho cha viongozi wa Palestina kupinga kuanzishwa uhusiano na Tel Aviv kinaenda kinyume na kanuni na kinapaswa kulaaniwa.

Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema matamshi hayo ya Bandar bin Sultan yametolewa kwa lengo la kuuhudumia utawala wa Kizayuni wa Israel.

Naye Saeb Erekat wa PLO kila Mwarabu anayetaka kujiuza kwa Marekani na wengineo na kila anayeunga mkono uhusiano wa kawaida na Israel afanye atakalo lakini asikosoe mapambano ya Wapalestina.

Mwanamfalme huyo amedai kuwa, "hatukutaraji haya kutoka kwa maafisa (wa Palestina) ambao wanataka kadhia yao ipate uungaji mkono wa kimataifa."

Bandar bin Sultan bin Abdulaziz ametoa matamshi ya kukinzana kwa kusema: Kadhia ya Palestina ni kadhia ya haki, lakini wanaoipigania ni watu waliofeli; na kadhia ya Israel si ya haki lakini watetezi wake wameonekana kufaulu. Huo ndio mukhtasarari wa matukio yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 70 hadi 75 iliyopita.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa utawala wa Riyadh ametoa kauli hiyo katika hali ambayo, ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu unaendelea kulaani hatua ya Imarati na Bahrain kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni.

Waislamu na wapenda haki kote duniani wamekitaja kitendo hicho cha UAE na Bahrain kama usaliti na ni sawa na kuwachoma jambia kwa nyuma wananchi madhulumu wa Palestina. 

3928343

captcha