IQNA

Maradona alikuwa muungaji mkono wa Palestina

20:46 - November 26, 2020
Habari ID: 3473396
TEHRAN (IQNA) - Mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Argentina Diego Maradona, aliyefariki Jumatano 25 Novemba akiwa na umri wa miaka 60 alikuwa muungaji mkono mkubwa wa Palestina.

Mwaka 2018, mjini Moscow, Maradona alikutana na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na huku akiwa amemkumbatia alimuambia ‘Moyoni Mwangu Mimi ni Mpalestina.”

Mwaka 2015 Maradona pia alitafakari kuhusu kuwa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Palestina katika Mashindano ya Bara Asia.

Kulingana na msemaji wake, Maradona amefariki dunia kutokana na mshutuko wa moyo, wiki mbili baada ya kuruhusiwa kutoka hopsitali. Mchezaji huyo aliyeiongoza Argentina kutwaa kombe la dunia mwaka 1986, alifanyiwa upasuaji wa ubongo mapema mwezi huu. 

Watu mashuhuri duniani na ulimwengu wa soka kwa ujumla, wanaomboleza kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona.

Aidha katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) Maradona anaombolezwa kutokana na uungaji mkono wake kwa watu wa Palestina na pia mitazamo yake ya kupinga vita vya Marekani dhidi ya Syria.

Katika moja ya mahojiano yake, Maradona alisema: “Hupaswi kuenda chuo kikuu kufahamu kuwa Marekani inalenga kuiangamiza Syria.”

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Sami Abu Zuhri ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Maradona na kusema: “Tumesikitishwa na kifo cha mmoja kati ya wachezasoka bora zaidi duniani, Maradona, ambaye alijulikana pia kuwa muungaji mkono wa ukombozi wa Palestina.”

captcha