IQNA

Mchambuzi: Kupokonya Silaha Harakati za Muqawama Ni Ndoto

19:19 - November 01, 2025
Habari ID: 3481446
IQNA – Kuzungumzia suala la “ Kupokonya Silaha Harakati za Muqawama” si chochote ila ni ndoto ya kufikirika, kwani maana yake ni kuwavua watu utashi wao na utambulisho wao, amesema mchambuzi wa kisiasa wa Kipalestina.

Silaha za Muqawama au harakati za Kiislamu za kupigania ukombozi zina hutumikia uhuru na heshima ya mataifa amesema Adnan Al-Sabah katika mahojiano na  Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) kuhusu hali ya hivi karibuni huko Gaza na hatua za utawala wa Kizayuni kwa baraka kutoka Marekani.

“Kwa hivyo, mradi uvamizi na uonevu vinaendelea, silaha za Harakati za Muqawama ni halali na ina mashiko,” alisisitiza.

Adnan Al-Sabah ni msomi mkongwe wa Kipalestina na mwandishi wa habari, pia ni mkuu wa Kituo cha Vyombo vya Habari cha Jenin. Alikuwa mwanzilishi na rais wa Kampeni ya Kimataifa ya Kurekodi Uhalifu wa Vita, na ni miongoni mwa waanzilishi wa Umoja wa Waandishi wa Kipalestina huko Al-Quds, ambako alihudumu katika bodi yake kwa vipindi kadhaa.

Mahojiano kamili ni kama ifuatavyo:

IQNA: Leo hii, baadhi ya tawala rasmi za Kiarabu zinategemea nafasi ya Marekani na mpango wa “amani” wa Trump. Unauonaje mpango huu? Je, unaweza kuleta mwisho wa vita na mwanzo wa amani kama wanavyodai wafuasi wake?

Al-Sabah: Mradi wa Marekani kimsingi umejengwa juu ya kutangaza vita dhidi ya dunia kutoka ndani ya dunia yenyewe. Marekani inatafuta kujenga dunia mpya; dunia chini ya utawala wake, si kwa kusimamia mahusiano ya usawa, bali kwa kuwala wengine. Hili la kutaka kutawala linaeleweka katika muktadha wa maendeleo ya zama za “maarifa”, ambapo uchumi wa maarifa umegeuzwa kuwa chombo cha ubeberu wa kiakili wa Marekani.

Kwa hivyo, Marekani haipaswi kuonekana kama inayotafuta amani; kinyume chake, inaweka misingi ya mtandao wa vita kwa sura na mifumo mipya. Vita kati ya Ukraine na Urusi ni “vita ya Marekani” inayopiganwa kwa kutumia mikono ya wengine: Ukraine inapigana kwa niaba ya Washington, Ulaya inalipa gharama, na faida za mwisho zinaingia hazina ya Marekani. Matokeo yake ni kudhoofika kwa Russia na wakati huo huo mmomonyoko wa kiuchumi wa Ulaya.

Katika Mashariki ya Kati, Marekani pia imebadilisha sura ya vita na kuunda migogoro ya bandia kati ya wahusika wa ndani , kati ya serikali ya Lebanon na Muqawama (Hizbullah), kati ya Ansarullah na mamluki huko Yemen, na kati ya serikali na vikosi vya Muqawama huko Iraq na Syria. Matokeo yake ni kuangamizwa kwa miundo ya kitaifa na kiuchumi ya nchi hizo na kupanuka kwa eneo la ushawishi wa moja kwa moja wa Marekani.

Washington inajaribu kufungua njia ya ardhini ya ushawishi wake kutoka Palestina iliyokaliwa hadi Kusini mwa Caucasus na nyuma ya ngome za Russia na Iran kupitia mipango kama “David Corridor” na “Zangezur Corridor”, mpango ambao kimakosa umeitwa “Mpango wa Amani wa Trump”. Katika Iraq na Iran, pia inatafuta kudhibiti na kudhoofisha mhimili wa upinzani kwa kuendeleza vikwazo na kuchochea migogoro ya ndani.

Kuanzia Amerika ya Kusini hadi Afrika, na kutoka Asia Kusini hadi Bahari ya Kusini ya China, Washington inajaribu kuwakabili na kuwachosha washindani wake wote , kutoka China hadi Ulaya, aidha kwa kuchochea migogoro (kama vile India na Pakistan, au Syria na Libya na Sudan) au kwa kuunda miungano ya kijeshi (kama AUKUS) ili kubaki kama kiongozi asiye na mpinzani katika mfumo wa dunia.

Trump ameeleza wazi falsafa hii: “Vita bora ni ile ambayo hushiriki lakini unashinda.” Wanataka amani kwa nguvu na kupitia kujisalimisha kwa wengine. Mipango yote hii ina lengo moja: kuangamiza mhimili wa upinzani na kuondoa nafasi ya Iran katika eneo, na hivyo kufungua njia kwa himaya ya Marekani.

3495220

Habari zinazohusiana
Kishikizo: muqawama silaha gaza
captcha