IQNA

Bomu laua watoto katika kikao cha kusoma Qur’ani Afghanistan

20:04 - December 18, 2020
Habari ID: 3473468
TEHRAN (IQNA) – Raia 15, wakiwemo watoto 11 wameuawa Ijumaa nchini Afghanistan baada ya bomu kulipuka katika kikao cha kusoma Qur’ani Tukufu kati mwa Afghanistan.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Tariq Arian, bomu liliwekwa katika tuk tuk katika mkoa wa Ghazni ambapo watu 20 walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa, mtu  ambaye alikuwa akiendesha tuk tuk aliingia katika kijiji cha Gilan kuuza bidhaa na punde alizingirwa na watoto waliotaka kununua bidhaa kisha bomu likalipuka

Hakuna aliyedai kuhusika na hujuma hiyo na serikali imesema uchunguzi unaendelea.

Msemaji wa wanamgambo wa Taliban Zabihullah Mujahid ametuma ujumbe kwa vyombo vya habari na kusema mlipuko huo umesababishwa na bomu ambalo halikuwa limelipuka  na kwamba watoto walilibeba na kumletea mwenye kuuza bidhaa katika Tuk Tuk na kisha mlipuko ukatokea.

Milipuko ya kigaidi imeongezeka miezi ya hivi karibuni nchini Afghanistan pamoja na kuwa mazungumzo baina ya wanamgambo wa Taliban na serikali ya Afghanistan yamekuwa yakifanyika nchini Qatar.

Tawkimu zinaonyesha kuwa machafuko yaliongezeka Afghanistan baada ya kufikiwa mapatano baina ya Marekani na kundi la Taliban mwezi Februari mwaka huu.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulionya kuhusu ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia na kutozingatiwa sheria za kibinadamu nchini Afghanistan.

Kundi la kigaidi la ISIS nalo limedai kuhusika na hujuma kadhaa dhidi ya maeneo ya raia ikiwemo misikiti nchini Afghanistan.

Marekani iliongoza waitifaki wake katika hujuma ya kijeshi Afghanistan Oktoba 2001 kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi. Hatahivyo ugaidi umeongezeka nchini humo na hadi sasa usalama haujaweza kupatikana. Uzalishaji wa dawa za kulevya nchini humo umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Katika mwaka 2000 na 2001, ukulima wa mihadarati Afghanistan ulikuwa ni tanu 200 lakini baada ya askari wa Marekani kuvamia nchi hiyo, kiwango hicho kimeongezeka na kufika takribani tani 10,000.

3473439

captcha