IQNA

Iran yalaani hujuma ya kigaidi Afghanistan iliyoua watu zaidi ya 30

16:54 - March 07, 2020
Habari ID: 3472542
TEHRAN (IQNA) - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amelaani shambulio hilo la kigaidi sambamba na kuwafariji wananchi na serikali ya Afghanistan pamoja na familia za waliouawa na kujeruhiwa katika hujuma hiyo.

Jana Ijumaa, watu zaidi ya 30 wameuawa na wengine 42 walijeruhiwa mjini Kabul, Afghanistan katika shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) katika shughuli ya hauli ya mwaka wa 25 tangu alipouawa shahidi aliyekuwa kiongozi wa chama cha Umoja wa Kiislamu cha Afghanistan, Abdul-ali Mazari.

Kiongozi nambari mbili wa serikali ya Afghanistan Abdullah Abdullah alikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria hauli hiyo, lakini alinusurika katika shambulio hilo.

Ripoti zinasema, watu 20 miongoni mwa waliojeruhiwa, wako mahututi.

Kundi la kigaidi la Daesh limekiri kuhusika na shambulio hilo la kinyama ambapo kwa mujibu wa tovuti ya kundi hilo ya Amaq jumla ya watu 150 waliuawa na kujeruhiwa katika hujuma hiyo.

Shambulio hilo ambalo lilitokea jana asubuhi limeelezwa kuwa la maafa makubwa zaidi tangu Marekani na kundi la Taliban ziliposaini makubaliano ya suluhu ya kuhitimisha vita vya zaidi ya miaka 18 vilivyotokana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Afghanistan. 

/3470847

captcha