IQNA

Waziri wa Palestina apokonywa pasi na Israel baada ya mkutano ICC

21:49 - March 22, 2021
Habari ID: 3473753
TEHRAN (IQNA)- Utawala haramu wa Israel umempkonya Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kibali maalumu kinachotumiwa na viongozi mashuhuru wa Palestina kuvuka mpakani, alipokuwa akirejea katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya kufanya kikao na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyo na makao makuu yake mjini The Hague Uholanzi.

Akifafanua suala hilo, Ahmed ad-Deek, afisa katika ofisi ya al-Maliki aliwaambia waandishi wa habari jana Jumapili kwamba Israel imechukua hatua hiyo kutokana na hatua ya al-Maliki ya kukutana na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Fatou Bensouda ofisini kwake huko Hague siku ya Alkhamisi.

Deek amelalamikia hatua hiyo na kusema Mamlaka ya Ndani ya Palestina inaichukulia kuwa ni shambulio na uchukozi wa moja kwa moja dhidi ya mamlaka hiyo kwa sababu Maliki si mtu binafsi bali ni kiongozi na mwakilishi wa serikali ya Palestina. Afisa huyo wa Palestina ameongeza kwamba maafisa wa Israel walizuia na kuwahoji wasaidi wa al-Maliki kwa muda wa dakika 90 katika kivuko kilichoko katika mpaka wa Jordan na Ukingo wa Magharibi.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Israel vimesema kuwa safari ya al-Maliki huko ICC ndiyo ilikuwa sababu ya yeye kupokonywa kibali hicho na askari wa Israel. Kibali hicho huwawezesha viongozi wa ngazi za juu wa Palestina kusafiri na kuvuka vizuizi vya mpakani vinavyodhibitiwa na wanajeshi wa Israel bila kukabiliwa na matatizo mengi.

Bensouda ametangaza kuwa ataanzisha rasmi uchunguzi katika tuhuma za jinai za kivita zilizotekelezwa na viongozi wa utawala wa kibaguzi wa Israel katika ardhi za Wapalestina. Ofisi ya al-Maliki ilisema Alkhamisi kuwa kiongozi huyo wa Palestina alikutana na kujadiliana na Bensouda juu ya udharura wa kuharakishwa uchunguzi huo.

Wataalamu wa masuala ya sheria wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza juu ya umuhimu wa kufanyika uchunguzi huo wakisema kuwa utawezesha Wapalestina wanaoteswa na kukandamizwa na utawala ghasibu wa Israel kufikia haki zao na uadilifu wa kisheria.

347429

Kishikizo: palestina icc israel
captcha