Baraza Kuu la Waislamu wa Kanada (NCCM) limetoa tamko rasmi likisifu tangazo hilo la serikali ya Kanada, likisema ni hatua iliyochelewa sana lakini hatimaye inatambua haki ya Wapalestina ya kujitawala.
“Hii ni siku ya kihistoria kwa Kanada,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NCCM, Stephen Brown, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Ottawa. “Tuna furaha kuona nchi yetu ikiungana na mataifa mengi duniani kuelekea kutambua rasmi mamlaka ya Palestina mwezi Septemba.”
Tangazo hili la Kanada linakuja wakati wa wito unaoongezeka kimataifa wa kusitisha mateso ya watu wa Palestina, hasa katika Ukanda wa Gaza ambako mashambulizi yanayoendelea ya Israel yamesababisha vifo vingi vya raia wasio na hatia—wakiwemo wanawake na watoto.
Uamuzi huu wa Kanada unatafsiriwa kama hatua inayoiweka pamoja na jumuiya ya kimataifa inayotambua kuwa mamlaka kamili ya Palestina ni msingi wa amani ya kudumu.
Brown alisisitiza kuwa haki ya Wapalestina kuwa na taifa lao haiwezi kujadiliwa. “Hatutakoma kutambua haki ya watu wa Palestina ya kuishi na kuwa na taifa huru, kujitawala, kupanga mustakabali wao, na kutumia haki yao ya asili ya kujitawala,” alisema.
Alikataa vikali hoja za kuchelewesha hatua hiyo akisema: “Hakuna sababu ya kuchelewa katika kutambua haki hii isiyoweza kuvunjwa... Uamuzi huu si wa kiishara tu.”
Brown alisisitiza uzito wa msimamo wa Kanada, hasa kwa kuzingatia “mauaji yanayoendelea” yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. “Mamlaka ya kujitawala ni nguzo muhimu ya maisha na heshima ya kila jamii – ikiwa ni pamoja na watu wa Palestina,” aliongeza.
Alitoa shukrani kwa Waziri Mkuu Mark Carney na viongozi wengine waliounga mkono hatua hiyo, lakini akasisitiza kuwa kutambua si mwisho, bali mwanzo wa hatua. “Israel bado inaendelea kuwanyima chakula na kuwaua Wapalestina, hususan watoto. Wakanada wengi hawaelewi vipi mateso haya yanaruhusiwa kuendelea bila kuchukuliwa hatua,” alisema kwa uchungu.
Kwa kuitaja kama wajibu wa kiutu na wa kimaadili, Brown alihimiza mipaka ifunguliwe ili misaada ya kibinadamu iweze kufika Gaza. “Wakihitaji msaada, sisi tupo tayari kuwasaidia,” alihitimisha.
3494073