IQNA

14:38 - July 17, 2021
News ID: 3474108
TEHRAN (IQNA)- Afisa mwandamizi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametoa wito kwa Waislamu kufuata mafundisho ya Qur’ani Tukufu ili kuweza kukabiliana na madola ya kibeberu.

Akizungumza Ijumaa katika sherehe za kufunga Mashindano ya Kwanza ya Kimataifa ya Qur’ani ya Oula-al-Qiblatain mjini Beirut, Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Hizbullah ya Lebanon, Sheikh Hashim Safiyyuddin, amesema: “Iwapo Waislamu wataifahamu vyema Qur’ani Tukufu na kutekeleza mafundisho yake, basi hakutakuwa na mifarakano na udhaifu katika ulimwengu wa Kiislamu.” Amesema iwapo Waislamu wataungana, basi watakuwa ummah mmoja na hawatakuwa chini ya satwa ya mabeberu.

Aidha amesema uingiliaji wa Marekani ndio sababu kuu ya masaibu yote ya Lebanon na akasisitiza kwamba, fitna ya Marekani inaandama na kuhujumu kila sehemu ya eneo la Asia Magharibi ulipo muqawama na uteteaji wa sharafu na heshima.

Hashim Safiyyuddin amefafanua kuwa, masaibu yote ya sasa ya Lebanon yamesababishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na Marekani.

Safiyyuddin ameongeza kuwa, Marekani imejiingiza Iraq, Afghanistan na Syria ili kuziangamiza nchi hizo; aidha inatuma silaha na makombora Yemen ili kuigeuza nchi hiyo magofu na kihame; na kwa kutumia vikwazo, inaiweka kwenye mashinikizo Lebanon na wananchi wengi wa mataifa mengine ya eneo.

Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Hizbullah ya Lebanon ameashiria maadhimisho ya ushindi wa muqawama katika Vita vya Siku 33 vya msimu wa joto wa mwaka 2006 na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na akasisitiza kwamba, leo muqawama uko imara zaidi katika upeo wa eneo, ukiwa na misingi imara na madhubuti zaidi na unazidi kukaribia kuyafikia malengo yake makuu.

Kwa mwaka mmoja na nusu sasa, Lebanon inakabiliwa na mgogoro kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kifedha na maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia ufisadi katika vyombo vya serikali. Marekani imekuwa ikihusika pakubwa katika kushadidisha matatizo ya kiuchumi ya Lebanon kwa hatua yake ya kidhalimu ya kuiwekea vikwazo vya kiuonevu harakati ya Hizbullah na viongozi kadhaa wa nchi hiyo.

3984497

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: