IQNA

Mkuu wa Al Azhar akosoa utumizi wa istilahi ya 'Dini ya Kiibrahimu'

16:43 - November 09, 2021
Habari ID: 3474533
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri Sheikh Ahmed el Tayyib, amekosoa jitihada za utumizi wa istilahi ya 'Dini ya Kiibrahimu' kwa lengo la kuziunganisha dini za Kiislamu, Kikristo na Kiyahudi.

Akizungumza katika kongamano chuoni Al Azhar Jumatatu, amesema jitihada kama hizo ni ndoto na zinalenga kuvuruga uhuru wa kuabudu. Amesema kulazimisha jambo hilo ni sawa na zile nadharia za 'utandawazi', 'mwisho wa historia' n.k.

Sheikh el Tayyib amesema wito huo wa 'Dini ya Kiibrahimu' kidhahiri ni wito wa umoja katika jamii ya mwanadamu kwa lengo la kuondoa mifarakano lakini dhati ya wito huo ni kufuta thamani za kidini na uhuru wa kuadudu.

Amesema uhuru huo wa kuabudu umedhaminiwa na kusisitizwa katika dini ambazo zinafuata itikadi ya Mungu moja.

Mkuu wa Al Azhar amesema haiwezekani watu kuafikiana kuhusu dini moja kutokana na hitilafu kuhusu imani na fikra.

Istilahi ya 'Dini ya Kiibrahimu' imekuwa ikihimizwa na kupigiwa debe sana siku hizi kwa lengo la eti kuziunganisha dini za Kiislamu, Kikristo na Kiyahudi.

Istilahi hii imetumiwa kuzishawishi nchi za Kiarabu kuanzisha mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ikumbukwe kuwa, ‘Mkataba wa Abraham (Ibrahimu)’ ulitiwa saini baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain ulitiwa saini tarehe 15 Septemba mwaka jana (2020) katika ikulu ya Marekani White House. 

4011745

captcha