IQNA

Majeshi ya majini ya Israel, Bahrain, UAE na Marekani yanafanya luteka ya pamoja

15:04 - November 12, 2021
Habari ID: 3474546
TEHRAN (IQNA)- Majeshi ya majini ya utawala haramu wa Israel, Bahrain, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu yamefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika Bahari ya Sham hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa pande hizo nne kukiri wazi kuwa zinafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.

Katika taarifa, Kamandi Kuu ya Jeshi la Majini la Marekani (NAVCENT), imetoa taarifa Alhamisi ikisema mazoezi hayo yalianza Alhamisi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mazoezi hayo ya siku tano yatajumuisha mafunzo katika meli ya kivita ya Marekani ya USS Portland na lengo lake ni kuimarisha ushirikiano baina ya wanajeshi wa nchi husika.

Afisa wa jeshi la majini la utawala haramu wa Israel  amewaambia waandishi habari kuwa kuanza kufanyika mazoezi kama hayo ya kijeshi chini ya usimamizi wa Marekani ni hatua katika kukabiliana na  ‘madhihirisho ya nguvu za Iran’ katika eneo.

Iran imekuwa ikitoa wito kwa nchi za eneo kutotegemea madola ajinabi kwa ajili ya kudhamini usalama  na kwamba usalama endelevu utapatikana tu kwa kushirikiana nchi za eneo. Aidha Iran inapinga hatua ya Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi zingine za Kiarabu ya kuanzisha uhusuano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Wananchi waliowengi katika mataifa ya Kiarabu pia wanapinga uamuzi wa tawala za nchi hizo kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israeli ambao unakoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina hasa mji wa Quds uliko Msikiti wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

 

4012473

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha