IQNA

Mkutano wa Umoja wa Kiislamu UAE waakhirishwa kutokana na aina mpya ya corona

16:45 - November 29, 2021
Habari ID: 3474618
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Jamii za Waislamu Duniani limeakhirisha Kongamano la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu la Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya kuibuka aina mpya ya kirusi cha COVID-19 ijulikanayo kama Omicron.

Baraza la Jamii za Waislamu Duniani limesema kongamano hilo ambalo lilikuwa lifanyike Disemba 12-14  chini ya anuani ya "Umoja wa Kiislamu, Fikra, Fursa na Changamoto", limeakhirishwa kufuatia kuibuka aina hiyo mpya ya corona.

Mwenyekitiw a baraza hilo Dkt. Ali Rashid Al Nuaimi amesema watatangaza tarehe mpya ya kongamano hilo baada ya janga la sasa kumalizika.

"Ingawa UAE ambayo ni mwenyeji haijakumbwa na aina hii mpya ya corona lakini hatua za tahadhari ambazo zimechukuliwa katika baadhi ya nchi zimepelekea safari kufungwa na hivyo takuwa vigumu kwa wageni kusafiri," ameongeza.

Baraza la Jamii za Waislamu Duniani ni taasisi ya kimataifa isiyo ya kiserikali yenye makao yake katika mji wa Abu Dhabi. Baraza hilo linajumuisha taasisi 900 za Kiislamu kutoka nchi 142 kwa lengo moja ambalo ni kujumuishwa jamii za Waislamu katika nchi wanazoishi huku wakizingatia mafundisho sahihi ya Kiislamu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa bado haijajulikana iwapo kiwango cha maambukizi ya kirusi kipya cha corona cha Omicron kitakuwa cha juu ikilinganishwa na aina nyingine kama ile ya Delta. Idadi ya watu waliofanyiwa vipimo vya corona katika nchi kadhaa za kusini mwa Afrika kufuatia kugunduliwa kirusi kipya inaendelea kuongezeka.

Hata hivyo tafiti  kuhusu magonjwa mbalimbali zinaendelea kufanywa ili kubaini iwapo maambukizi yanayoongezeka yanatokana na aina hiyo mpya ya Omicron au la. Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa bado haijafahamika iwapo spishi mpya ya kirusi cha corona aina ya Omicron inasababisha kuongezeka maambukizi au vifo.  

3476706

captcha