IQNA

Mwanazuoni aeleza Jinsi Mtume Muhammad (SAW) Alivyounda Umma mmoja kutoka jamii ya kikabila

16:17 - August 22, 2025
Habari ID: 3481122
IQNA – Mwanazuoni kutoka Iran amesisitiza mafanikio ya kihistoria yaliyopatikana na Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kwa kuunda Umma mmoja ulioshikamana, kutoka jamii za kikabila zilizokuwa zikitumbukia katika migawanyiko na mifarakano.

Hujjatul Islam Seyed Ali Akbar Norui, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Jamiat al-Zahra (AS), alisema katika mahojiano na IQNA , yaliyofanywa katika kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad (SAW) kwamba mafanikio hayo yalitokana na mchanganyiko wa sababu za kimaadili, kijamii na kiakili.

Alibainisha kwamba upole wa Mtume (SAW), msamaha wake, kumuombea msamaha mwingine, kushauriana na watu, tabia yake tukufu, heshima aliyokuwa nayo kabla ya kutumwa, pamoja na hekima na busara yake, vilikuwa miongoni mwa nguzo kuu zilizochangia kuundwa kwa taifa moja la Kiislamu lililoungana.

“Tabia hizo ndizo zilizosababisha watu wenye tamaduni na desturi tofauti, hata makabila na koo zilizokuwa na migongano, kuungana chini ya uongozi wa Mtume Mtukufu (SAW),” alisema.

Mwanazuoni huyo aliongeza kuwa katika aya ya 159 ya Surah Aal-Imran, Mwenyezi Mungu anamkumbusha Mtume (SAW) kwamba siri ya watu kuungana na kumzunguka ilikuwa ni hulka yake ya upole, ustahimilivu na huruma.“Kama Mtume (SAW) angelikuwa mkali na mwenye moyo mgumu, watu wangelimkimbia.”

Hujjatul Islam Norui alifafanua kuwa kulikuwa na mambo matatu makuu yaliyochangia kuvuta nyoyo na kujenga mshikamano kupitia mwenendo wa Mtume (SAW):

1.    Msamaha na kuwasamehe watu kwa makosa yao, jambo lililowavutia na kuwapa imani kwake.

2.    Kuuombea msamaha umma wake mbele ya Mwenyezi Mungu, ishara ya huruma na kujali ustawi wa wengine.

3.    Kuwashirikisha katika mashauriano ya kijamii, kulikowapa hadhi na nafasi ya kushiriki maamuzi ya pamoja.

Sifa hizi, zikiwa zimeunganishwa na upole na wema, ziliunda msingi madhubuti wa mshikamano wa kijamii.

Aidha, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa na hekima isiyolinganishwa na uhodari, na kwa mwongozo wa Mwenyezi Mungu aliweza hatua kwa hatua kuondoa vikwazo vya umoja miongoni mwa koo zilizokuwa zimegawanyika, huku jamii hiyo ya wakati huo ikiwa imezongwa na chuki na uadui wa kikabila uliodumu kwa vizazi.

Bila shaka haimaanishi kuwa hakukuwa na tofauti ndani ya Umma, lakini Mtume Muhammad (SAW) aliweza kuunda jamii iliyo thabiti, jeshi lililoshikamana lililoshinda Makka na kulinda mipaka ya Uislamu, na hatimaye kuunda taifa moja lenye mshikamano.

Alipoulizwa kuhusu ni kipi cha maisha ya Mtume (SAW) kinachoweza kutoa mwongozo kwa ulimwengu wa kisasa, alisema:“Hakika ukweli wa mwanadamu haujabadilika jana, leo wala kesho. Mahitaji yake ya kimwili na ya kiroho ni yale yale. Hatuwezi kudhania kuwa sehemu ya Uislamu pekee ndiyo tiba, bali ni Uislamu mzima unaopaswa kutekelezwa katika jamii za kibinadamu wakati wowote ili kuondoa maumivu ya mwanadamu.”

Aliongeza: “Iwapo tunataka jibu sahihi, tunapaswa kurejea kwenye aya za Qur’ani kama vile aya za 10 na 11 za Surah As-Saff. Aya hizi zinaonesha tiba ya matatizo ya mwanadamu: kwanza kukubali na kumwamini Mwenyezi Mungu, pili kumwamini Mtume Wake (SAW), kisha kujitolea nafsi na mali katika njia ya Mwenyezi Mungu.Njia hii humwokoa mwanadamu kutokana na taabu na hofu, humfikisha kwenye pwani ya amani na kumkimu kwa mahitaji yake ya kimwili na kiroho.”

Alipoulizwa kuhusu ujumbe wa Mtume (SAW) kwa dunia ya leo iliyojaa migogoro ya kimaadili na kijamii, Hujjatul Islam Norui alisema:“Bila imani kwamba Mwenyezi Mungu anamjali mwanadamu na tayari amemwekea suluhu, matatizo ya mwanadamu hayatapata tiba. Maelekezo ya uponyaji wa maradhi ya mwanadamu – yale ya jana na ya leo – yameelezwa wazi katika Qur’ani Tukufu.”

Alinukuu Aya ya 64 ya Surah Aal-Imran:“(Ewe Muhammad), waambie Watu wa Kitabu: Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu.”

Mwanazuoni huyo alihitimisha kwa kusema:“Ujumbe wa Mtume Mtukufu (SAW) kwa dunia ya sasa ni kumtambua Mwenyezi Mungu na Mitume Wake katika maisha yetu; kwamba hakuna binadamu aliye bora juu ya mwenzake; kwamba wote ni sawa – waja wa Mwenyezi Mungu. Maisha yanapaswa kuwa ya uadilifu, na matatizo ya kijamii na kiuchumi yashughulikiwe kwa hekima na mizani ya haki.Utekelezaji wa kanuni hizi ndio utakaoikomboa dunia kutoka migogoro ya kimaadili na kijamii na kuielekeza kwenye mustakabali wa amani na mwanga. Hatimaye, utekelezaji wake kamili unahitaji kuja kwa Mkombozi wa kweli (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) na utayari wa wanadamu kumpokea.”

3494351

captcha