IQNA

Jinai za Israel

Wapalestina waandamana kulaani safari ya Biden Asia Magharibi

12:23 - July 15, 2022
Habari ID: 3475504
TEHRAN (IQNA)- Mamia ya Wapalestina wamefanya maandamano katika eneo la kaskazini la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kupaza sauti zao za kupinga ziara ya Rais Joe Biden wa Marekani katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina la Israe katika safari yake ya kwanza ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kama rais wa Marekani.

Waandamanaji hao walikusanyika kwenye Uwanja wa Mashahidi mjini Nablus, ulioko takriban kilomita 49 kaskazini mwa al-Quds (Jerusalem), Alhamisi alasiri katika maandamano yaliyoandaliwa na Kamati ya Uratibu ya Makundi ya Palestina.

Wapalestina hao walisikika wakitoa nara dhidi ya Marekani za kupinga safari ya Biden, na kukemea sera za wazi za Washington za kuupendelea utawala ghasibu wa Israel.

Nasser Jawabreh, mjumbe mkuu wa Kamati ya Uratibu wa Makundi ya Palestina alisema katika hotuba yake katika hafla hiyo kwamba taifa zima la Palestina, mirengo na taasisi za kisiasa zinapinga safari ya rais huyo mwenye umri wa miaka 79 kwa vile anaunga mkono wazi wazi utawala bandia wa Israel.

Wakati huo huo  Bassem Na'aim, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu, Hamas, amesema Rais wa Marekani hana suluhu la mzozo wa Palestina na Israel. Naye Ahmad Al-Medalal, mwanachama wa harakati ya Jihadi ya Kiislamu alisisitiza kwamba Wapalestina hawapaswi kutegemea "mradi wa Marekani katika eneo."

Amesema uongozi wa Palestina lazima uunde safu ya kitaifa ili kukabiliana na utawala wa Israel.

Maher Mezher, kiongozi wa  Chama cha Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina (PFLP), pia amesema kuwa ziara ya Biden inalenga kuimarisha ubeberu wa Marekani katika eneo hilo.

Wakati huo huo vyama kadhaa vya siasa nchini Misri vimetangaza kuwa vinapinga kuanzishwa aina yoyote ya muungano wa kijeshi kati ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa hatua kama hiyo itahatarisha amani na usalama wa kimataifa.

Vyama vya siasa vya upinzani nchini Misri vinavyojumuisha Al Karamah, Ad-Dustur, Muungano wa Wananchi, Demokrasia ya Kijamii, Wahafidhina, Uadilifu, Al Aish na Al Hurriyah vimesisitiza katika taarifa yao ya pamoja kuwa, kabla ya kufanyika kikao cha siku ya Ijumaa cha viongozi wa nchi za Kiarabu na Marekani katika mji wa Jeddah Saudi Arabia, vinatangaza rasmi na kinagaubaga kuwa vinapinga vikali nchi za Kiarabu kuanzisha muungano wa aina yoyote na utawala wa Kizayuni kwa kutumia anuani au kisingizio chochote kile.

Katika taarifa yao hiyo, vyama hivyo vya upinzani nchini Misri vimeeleza bayana kuwa, kuna fursa nyingi za kujenga maelewano kati ya nchi za Kiarabu na Iran katika ngazi na nyuga zote.

Sambamba na kuanza ziara ya rais Joe Biden wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, kwa mara nyingine tena zimekuwa zikisikika kutoka kwa baadhi ya viongozi wa nchi za eneo na pia katika vyombo vya habari kauli za kuasisiwa NATO ya Kiarabu. Biden anatazamiwa kukutana na viongozi wa nchi kadhaa za Kiarabu huko Jeddah, Saudi Arabia kujadili mkakati huo wa kuunda muungano wa kijeshi.

3479702

captcha