IQNA

Kadhia ya Palestina

Viongozi wa nchi za Kiarabu wataka uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina ukomeshwe

13:22 - November 03, 2022
Habari ID: 3476028
TEHRAN (IQNA) – Washiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Algeria wamesisitiza ulazima wa kukomesha uvamizi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Palestina.

Mkutano huo ulianza Jumanne kwa kushirikisha wakuu wa nchi na maafisa wengine wakuu kutoka nchi za Kiarabu pamoja na wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa, akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Ukiwa na kauli mbiu ya umoja, ni mkutano wa kwanza wa kilele wa Jumuiya ya Waarabu tangu kuzuka kwa janga la COVID-19.

Hati inayoitwa Azimio la Algeria ambayo iliandaliwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama hapo awali pia inajadiliwa katika mkutano huo.

Suala la Palestina ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vilivyotajwa katika waraka huo, ambao pia una mapendekezo kuhusu migogoro katika nchi sita za Kiarabu.

Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano huo, alisema katika hotuba ya ufunguzi kwamba mkutano huo unafanyika katika hali nyeti na ngumu katika kanda na kwingineko.

Pia alitoa wito wa kuundwa kambi ya kiuchumi ya Waarabu kwa ajili ya kulinda maslahi ya pamoja pamoja na kufanya mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kujadili kadhia ya kuipa Palestina uanachama kamili.

Katibu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit katika hotuba yake alisisitiza haja ya kukomesha mgogoro wa Syria na juhudi za kurejesha nchi hiyo kwenye Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alizungumza kwenye hafla hiyo, akisema msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina ni kwamba ukaliaji wa mabavu wa Palestina lazima ukomeshwe.

Rais mpya wa Iraq, Abdul Latif Rashid, katika hotuba yake alitoa wito kwa nchi za Kiarabu kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo. Mkutano huo wa kilele nchini Algeria utakamilika leo.

Jumuiya ya Kiarabu ni shirika la kitaifa la kikanda la nchi zinazozungumza Kiarabu katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka wa 1945, yenye makao yake makuu mjini Cairo inasema dhamira yake ni kukuza biashara na ukuaji wa uchumi pamoja na uhuru na utulivu wa kisiasa katika eneo hilo.

4096425

captcha