IQNA

Mpango wazinduliwa kuhusu kuandika wasifu wa maulamaa 84,000 wa Kiislamu

15:51 - October 04, 2025
Habari ID: 3481326
IQNA – Mpango kabambe wa utafiti wa maisha ya maulamaa 84,000 wa Kiislamu umezinduliwa rasmi, kwa mujibu wa msomi wa Kiislamu kutoka Iran.

Juhudi hizi zinalenga kukusanya na kuchambua rekodi za kimaisha, kifikra, na kiakhlaqi za maulamaa wa Kiislamu katika historia, kwa madhumuni ya kuunda mfumo wa kitaalamu wa utafiti wa baadaye na kuhifadhi utamaduni wa Kiislamu. Mradi huu unatarajiwa kuhitimishwa kwa kuanzishwa kwa kile waandaaji wanakitaja kuwa makumbusho makubwa zaidi ya maulamaa wa Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hujjatul-Islam Hamid Mohammadi, mjumbe wa baraza la sera la kongamano hilo, alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran kuwa “kuchunguza maisha ya baraka ya maulamaa wa Kiislamu ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo yamepuuzwa kwa muda mrefu.”

Alibainisha kuwa timu ya utafiti hadi sasa imechambua vichwa 33,000 vya wasifu kutoka maisha ya maulamaa, kwa lengo la kuyatumia kama mifano ya malezi na mwongozo wa kijamii.

“Tumeandaa orodha pana ya maulamaa waliokuwa na mchango katika nyanja za kisiasa, na kwa mara ya kwanza tumeanzisha makundi mapya kadhaa ya uainishaji,” alisema.

Mohammadi alieleza kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha uchunguzi wa maulamaa 84,000 wa kidini ndani ya makundi hayo 33,000. Lengo kuu, aliongeza, ni kujenga hifadhidata kubwa itakayokuwa msingi wa makumbusho na maktaba ya kidijitali.

Alisema mradi huo unachunguza vipengele vinne muhimu — mazingira ya maisha, fikra, kauli, na vitendo vya maulamaa — na tayari umebaini taasisi 1,100 zinazofanya kazi katika eneo hilo.

“Tangu mwaka 2018, tumepanga takriban nukta milioni 80 za data, na hatua inayofuata ni kuunda algorithimu za kuoanisha taarifa hizi na Qur’an, Hadith, na urithi wa maulamaa mashuhuri,” alieleza.

Kwa mujibu wa Mohammadi, lengo la muda mrefu ni kupanua ukusanyaji wa data hadi kufikia rekodi bilioni 1.5, ili kuwezesha uchambuzi wa kina na uundaji wa mifano ya maarifa. “Kupitia kongamano hili, tunatoa mwaliko kwa wanafikra na maulamaa wenye uchungu kutoka ulimwengu mzima wa Kiislamu,” aliongeza.

Alieleza pia mipango ya kutumia matokeo ya utafiti huo katika mazingira ya kazi na elimu, akisema kuwa hatua muhimu zaidi itakuwa utekelezaji wa matokeo hayo kwa vitendo.

Kongamano la kimataifa limepangwa kufanyika Oktoba 23, huku makala 80 za utafiti zikiwa tayari zimewasilishwa.

Mohammadi alisisitiza kuwa ulimwengu wa Kiislamu una “urithi tajiri wa ustaarabu,” na kwamba kugundua upya urithi wa kiakili na kiakhlaqi wa maulamaa wake kunaweza kusaidia kuimarisha misingi ya kitamaduni na kielimu kwa vizazi vijavyo.

3494864

Kishikizo: qurani tukufu maulamaa
captcha