IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /36

Yunus; Nabii aliyehukumu kabla ya wakati wake

15:31 - April 06, 2023
Habari ID: 3476820
TEHRAN (IQNA) – Baada ya kuona dalili za adhabu ya Mwenyezi Mungu, watu wa Nabii Yunus walitubu lakini Yunus (AS) hakusubiri na akasisitiza juu ya adhabu yao. Kwa hiyo, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, nyangumi akammeza Yunus (AS).

Yunus (AS), mtoto wa Matta alikuwa nabii wa Bani Isra’il ambaye aliteuliwa mtume baada ya Suleiman (AS). Baadhi ya wanahistoria wanasema alikuwa dhuria wa Ibrahim (AS) wakati wengine wanaamini kuwa alikuwa wa ukoo wa Yaqub (AS). Bado baadhi ya wanahistoria wengine wanasema alikuwa dhuria wa Hud (AS) na mama yake alitoka Bani Isra’il. Aliishi katika karne ya 8 KK huko Nineveh, Iraq

Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, aliwaalika watu wa Nineveh kwenye imani ya Mungu mmoja lakini waliukataa wito wake. Hivyo, Mwenyezi Mungu alimjulisha juu ya adhabu iliyokuwa karibu. Alipoona mawingu mekundu angani, ambayo yalikuwa ishara ya kuja kwa adhabu, Yunus aliondoka mjini.

Mfalme wa Nineveh alikusanya wanaume, wanawake na watoto ili kumwambia Yunus kwamba wanataka kutubu na kuwa na imani kwa Mungu. Lakini Yunus alikuwa tayari ameondoka.

Yunus alikasirika kuona kwamba watu walitaka kuwa na imani katika dakika ya mwisho tu na baada ya kuona dalili za adhabu. Alienda baharini ili watu wasimwone. Aliapa kutorejea tena mjini.

Watu pia waliondoka mjini. Mfalme alimwomba Mungu aondoe adhabu hiyo, akisema, “Ikiwa mjumbe wako ametuacha, wewe hutatuacha. Ingawa tumepoteza matumaini kwa nabii wako, hatutapoteza matumaini kwako.”

Mfalme na watu walilia na kumwomba Mungu kwa muda wa siku nne mpaka Mungu alipokubali toba yao na kuwaondolea adhabu.

Imesemekana kwamba Mwenyezi Mungu akitaka kuwaadhibu watu hatawaondolea adhabu hata wakitubu katika dakika za mwisho, lakini kisa cha watu wa Yunus kilikuwa ni cha pekee.

Baharini, Yunus alipanda meli. Siku moja, dhoruba kali ilipiga meli hiyo. Wafanyakazi na abiria walianza kuhofia maisha yao huku maji ya bahari taratibu yakianza kumiminika kwenye sitaha na kuizamisha meli taratibu. Wafanyakazi walitupa mzigo wa ziada wa meli; lakini, meli iliendelea kuzama kwani bado ilikuwa nzito sana. Nahodha hakuwa na la kufanya—ilimbidi atoe uhai wa mtu mmoja ikiwa angetaka kuokoa maisha ya wafanyakazi wake na abiria. Kwa kuwa ilikuwa kawaida nyakati hizo, nahodha aliamua kupiga kura kuchagua abiria wa kutolewa muhanga.

Kura zilipigwa na jina la Nabii Yunus likachaguliwa. Wanaume hao walijua kwamba Yunus alikuwa kijana, mwadilifu, mwaminifu na mtu aliyebarikiwa, hivyo walikataa kumtupa nje na wakakubali kupiga kura tena. Kwa hivyo kura zilipigwa, na jina la Yunus likatokea tena. Waliokuwa hapa walikataa kumtupa baharini. Kwa hiyo wakapiga kura kwa mara ya tatu, na jina la Yunus likatokea tena! Watu walichanganyikiwa, lakini Nabii Yunus akajua kwamba hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa amewaacha watu wake bila ya ridhaa ya Mola wake. Kwa hiyo Yunus akaruka kutoka kwenye meli kwenye giza.

Kama Mungu alivyoamuru, nyangumi mkubwa zaidi katika bahari alimmeza Yunus mara tu alipopiga maji. Yunus ambaye alikuwa amepoteza fahamu alizinduka na kujikuta amegubikwa na giza totoro.

Yunus alikuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa muda wa siku 40, akimuomba Mwenyezi Mungu mpaka maombi yake yakajibiwa na nyangumi akaogelea hadi ufuo wa karibu na kumtoa Yunus.

Baada ya kupata nafuu, Yunus alipewa kazi ya kurudi Nineveh na kuwaongoza watu.

Jina la Mtume Yunus (AS) limetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu mara nne. Sura ya kumi ya Qur'ani Tukufu pia imepewa jina lake.

 

captcha