IQNA

Milad un Nabii

Raisi wa Iran azindua toleo la tano la Tuzo ya al Mustafa (SAW)

20:18 - September 30, 2023
Habari ID: 3477671
TEHRAN (IQAN)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika toleo la tano la Tuzo ya al Mustafa (SAW) kuwa sayansi na elimu yenye manufaa ni elimu inayosababisha saada na ufanisi kwa mwanadamu na kuongeza kuwa, tangu hapo awali, Wamagharibi walikuwa na wasiwasi kwamba kutajitokeza ustaarabu mpya wa kukabiliana nao, na hii ndiyo sababu kuu ya chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na chuki dhidi ya Iran (Iranophobia).

Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika sherehe hizo kwamba mkutano huu ambao umeandaliwa chini ya kivuli cha jina la al Mustafa (SAW) kwa ajili ya kuenzi na kuadhimisha nafasi ya elimu na maarifa, ni kielelezo kwamba moja kati ya sifa za Mtume Muhammad (SAW) ni "al Muhaimin" kwa maana ya kulinda na kusimamia viumbe vyote. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nafasi ya kisayansi na kielimu ya Mtume Muhammad (SAW) ndiyo ya juu kabisa, na kuongeza kuwa, Mtume (SAW) kama mtu mwenye elimu zaidi kati ya walimwengu, anaifafanua sayansi na elimu akisema: "Sayansi iko katika mambo matatu, fikra na kumwamini Mwenyezi Mungu, maadili mema na katika mtindo wa maisha wa mwanadamu anayeelekea kwa Mwenyezi Mungu. Katika maelezo hayo, maarifa au sayansi yenye manufaa ni ile inayotumika kwa ajili ya saada na ufanisi wa mwanaadamu na kufungua mafundo katika maisha ya wanaadamu."

Rais Ebrahim Raisi  amesisitiza kuwa, elimu na sayansi inayotumiwa kwa ajili ya kujipata madaraka, utajiri, ukoloni na unyonyaji, itasababisha maangamizi ya wanaadamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Katika historia ya Uislamu, tunaona kwamba ustaarabu wa Kiislamu ulianzishwa sambamba na mwanzo wa ujumbe wa Mtume, na harakati hii ya kisayansi iliibua mwamko katika karne ya tatu na nne katika Ulimwengu wa Kiislamu ambao ndiyo chimbuko la sayansi na ustaarabu wa Ulaya.

Sayyid Ebrahim Raisi ameendelea kwa kusema kuwa, tuzo ya al Mustafa sio tuzo ya sayansi pekee, bali ina mbawa mbili za sayansi, imani na dini, na kusema kuwa, ujumbe wa tuzo ya al Mustafa ni kuwa na ustawi, saada na ustaarabu wa mpya wa binadamu.

Tuzo ya Mustafa hutolewa katika uwanja wa fizikia kwa wanasayansi bora wa Kiislamu ambao wanaishi na kufanya kazi ndani ya nchi za Waislamu na nje ya nchi hizo.

Tuzo hii ya aina yake katika ulimwengu wa Kiislamu hutolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kila baada ya miaka miwili kwa wasomi na wanasayansi bora wa Ulimwengu wa Kiislamu waliovumbua mambo mbalimbali katika masuala ya elimu na sayansi kwa ajili ya kuboresha maisha ya mwanaadamu.

Tuzo ya Sayansi ya Mustafa SAW (The Mustafa (PBUH) Prize) ilizinduliwa mwaka 2013 na ilitolewa mara ya kwanza mwaka 2015 mjini Tehran.

3485368

Kishikizo: mustafa Mustafa Prize
captcha