IQNA

Dini

Ayatullah Khamenei: Heshima kwa Nabii Isa (Yesu) ni suala la yakini miongoni mwa Waislamu

20:58 - July 30, 2024
Habari ID: 3479204
IQNA – Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyed Ali Khamenei amesisitiza jinsi Waislamu wanavyomheshimu Nabi Isa au Yesu – Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake-(AS), huku akikemea kudhalilishwa kwa mtume huyo Mwenyezi Mungu.

Imam Khamenei aliyasema hayo katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan na ujumbe alioandamana nao leo jijini Tehran.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina sera madhubuti na imara ya kupanua uhusiano na majirani zake hususan Armenia. "Tumejitolea kwa dhati kuendeleza uhusiano na Armenia, na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaendelea kwa msingi wa masilahi yaliyofafanuliwa, bila kujali sera za wengine."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa shukurani zake kwa kuhudhuria kwa Bwana Pashinyan katika hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran Daktari Masoud Pezeshkian, na katika mazishi ya Shahidi Rais Ebrahim Raisi. Amesisitiza umuhimu wa kudumisha mamlaka ya kujitawala Armenia na akaongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauona ukanda wa Zangezur kuwa na madhara kwa Armenia, na kwa inasisitiza msimamo wake thabiti kuhusu suala hili.

Imam Khamenei amesisitiza kuwa, madola ya kigeni hayapaswi kuweka vikwazo katika uhusiano kati ya nchi na majirani zao.  Ameongeza kuwa kinachohakikisha usalama na ustawi wa mataifa ni kujitegemea na kuwa na washirika wa karibu.  Aidha alibainisha kuwa vitendo vya baadhi ya wanaoingilia  masuala ya nchi nyingine kutoka mbali hatimaye hudhuru nchi hizo.

Kiongozi Muadhamu ameashiria pia uhusiano mzuri uliopo kati ya Wairani na jamii ya Waarmenia ndani ya Iran na kusisitiza kuwa, "Waarmenia nchini Iran walikuwa na nafasi kubwa wakati wa vita vya kulazimishwa (vya Iraq dhidi ya Iran), na mimi binafsi nimetembelea nyumba za Waarmenia wengi."

Imam Khamenei amesisitiza heshima kwa Nabii Isa (AS) kuwa ni suala la yakini la lisilopingika miongoni mwa Waislamu. "Tunalaani matusi yanayoelekezwa kwa shakhsia wa dini za Mwenyezi Mungu, akiwemo Isa Masih (Yesu Kristo)."

Imam Khamenei alikuwa akiashiria matusi na kuvunjiwa heshima Nabii Isa (AS)  katika sherehe za uzinduzi wa Olimpiki ya Paris ya 2024.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Mohammad Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa Rais Pashinyan alielezea kuridhishwa na uhusiano unaokua kati ya Tehran na Yerevan. Alielezea majadiliano yake na Rais wa Iran Dk. Masoud Pezeshkian kuwa yenye kujenga na chanya.

Bwana Pashinyan aliutaja uhusiano kati ya Iran na Armenia kuwa wa kistratijia na kueleza furaha yake kutokana na kupanuka na kutofautisha uhusiano wa nchi hizo mbili. Alisisitiza umuhimu wa kudumisha mwelekeo huu mzuri.

 Chanzo: Khamenei.ir

3489304

captcha