IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Uswidi yamshtaki Mdenmark aliyevunjia heshima Qur’ani Tukufu

20:44 - August 09, 2024
Habari ID: 3479250
IQNA - Uswidi  (Sweden) imemshtaki mwanamume wa miaka 42 kutoka Denmark kwa uchochezi dhidi ya jamii moja (Waislamu) na matusi siku ya Jumatano, waendesha mashtaka walisema katika taarifa.

Ingawa Mamlaka ya Mashtaka ya Uswidi haikumtaja mshukiwa huyo, vyombo vya habari vya Uswidi, vikiwemo Dagens Nyheter, Sveriges Radio, na Aftonbladet, vimemtambua kuwa Rasmus Paludan, mfuasi wa itikadi kali Mswidi-Mdenmark ambaye katika miaka michache iliyopita alivutia hisia za kimataifa kwa vitendo vyake vya kuteketeza moto nakala za Qur'ani hadharani.

Taarifa hiyo ilisema mashtaka yanahusiana na matukio mawili ya Aprili na Septemba 2022 huko Malmö. Paludan alikuwa amehudhuria mikusanyiko ya hadhara katika mji wa Uswidi nyakati hizo zote mbili, ambapo alitoa maoni ya chuki yaliyoelekezwa kwa Waislamu, Waarabu na Waafrika.

"Tathmini yangu ni kwamba kuna sababu za kutosha za kuleta mashtaka, na sasa mahakama ya wilaya itazingatia kesi hiyo," mwendesha mashtaka mkuu Adrien Combier-Hogg alisema.

Paludan, mwenyekiti wa chama cha siasa kali mara kadhaa amekuwa akichoma moto nakala za Qur’ani katika miji ya Stockholm na Copenhagen, na hivyo kuzua hasira katika nchi zenye Waislamu wengi. Nchini Iraq, mamia ya watu walivamia Ubalozi wa Uswidi mjini Baghdad wakipinga vitendo vya uchomaji wa nakala za Qur’ani.

Mnamo Aprili 2022, wimbi kali la ghasia lilienea nchini Uswidi kujibu mikutano iliyoandaliwa na Paludan ambapo alipanga kuchoma nakala ya Qur’ani.

3489424

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu uswidi
captcha