
Akipokelewa na Safi Arpaguş, Rais wa Masuala ya Kidini Uturuki (Diyanet), Papa alivua viatu na kutembea ndani ya msikiti uliotandikwa mazulia, akitazama vigae vya samawati na kuba kubwa lililoinuka juu.
Msikiti huo ulijengwa mwaka 1617 chini ya utawala wa Sultan Ahmed I, na ni alama muhimu ya usanifu wa Kiislamu wa Kiosmani, ukiendelea kuwa kituo cha ibada kwa Waislamu wengi wa Istanbul.
Imamu wa msikiti, Asgin Tunca, aliwaambia waandishi wa habari kuwa alimueleza Papa kuwa “hii ni nyumba ya Mwenyezi Mungu,” na akaongeza: “Ikiwa unataka, unaweza kuabudu hapa.” Kwa mujibu wa imamu, Papa alikataa lakini alieleza kuwa alitaka “kuona msikiti” na “kuhisi mazingira yake.”
Kwa muda mrefu, Msikiti wa Sultan Ahmed umekuwa sehemu ya ratiba za mapapa wa kisasa kama ishara ya heshima kwa Waislamu. Papa Leo ameendeleza utamaduni huo, ingawa aliondoa Hagia Sophia katika ratiba yake. Kanisa hilo la zamani la Bizanti lilibadilishwa tena kuwa msikiti mwaka 2020, jambo lililokosolewa na baadhi ya serikali za Magharibi na Vatican.
Ziara ya Papa katika Blue Mosque ilianza siku iliyotengwa kwa mawasiliano ya kidini. Baada ya kuondoka, alikutana kwa faragha na viongozi wa jumuiya za Kikristo za Uturuki katika Kanisa la Kisyriani Othodoksi la Mor Ephrem. Baadaye, alitarajiwa kushiriki sala na Patriarki wa Kiekumeni Bartholomew I katika Kanisa la Othodoksi la Kipatriarki la Mtakatifu George.
Ziara hii inakuja katika juhudi pana za Papa za kukuza mazungumzo kati ya jumuiya za kidini duniani. Ijumaa, alijiunga na viongozi wa Kikristo mjini Iznik, Nicaea ya kale, kuadhimisha miaka 1,700 ya Baraza la Nicaea, mkutano muhimu uliotoa Nicene Creed ambayo bado inasomwa na madhehebu mengi ya Kikristo.
Papa aliwasihi viongozi “kushinda fedheha ya migawanyiko” na kuimarisha umoja katika wakati wa migogoro ya kibinadamu duniani.
Papa Leo atahitimisha siku yake Istanbul kwa kusalia Misa na Wakatoliki wachache wa Uturuki, wanaokadiriwa kuwa takriban 33,000 kati ya idadi ya watu zaidi ya milioni 85.
3495554