
Mtunzi huyo mashuhuri wa India alifanya kazi na mtengeneza filamu wa Iran Majid Majidi na kuandika wimbo wa filamu yake, Muhammad: Mtume wa Allah. Filamu hiyo ilitolewa mwaka wa 2015, na kuwa filamu ya pili kutayarishwa kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (SAW) baada ya The Message ya Mustafa Akkad mwaka 1976.
Kwa mnasaba wa Maulid au siku ya kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) limezungumza naye A. R. Rahman kuhusu filamu hii na pia mapenzi kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).
A. R. Rahman ni mtunzi wa India, mwimbaji, na mtunzi wa nyimbo anayejulikana kwa kazi yake katika filamu za Kitamil na Kihindi, pamoja na kazi zake nyingine kimataifa. Ameshinda tuzo nyingi, ikiwa ni pamoja na Tuzo mbili za Academy kwa kazi yake kwenye filamu "Slumdog Millionaire" (2008) na "Jai Ho."
Rahman pia amepokea Golden Globe na tuzo ya BAFTA kwa filamu hizo. Muziki wake wa kibunifu unachanganya vipengele vya muziki wa kitamaduni, vya kielektroniki, na miziki ya maeneo mengine duniani hivyo kumfanya atambulike kimataifa na sifa nyingi.
Haya hapa mahojiano hayo.
IQNA: Ni nini kilikupa msukumo katika kutunga muziki wa filamu ya Muhammad: Mtume wa Allah?
Rahman: Nilipigiwa simu na rafiki yangu ambaye alisema kwamba Bwana Majidi anataka kukutana nami. Na huko India, nadhani Majid ni mtegeneza filamu mashuhuri kwani filamu yake ya "Watoto wa Mbinguni" ni mashuhuri kwani ilifungua hisia za watu kuhusu filamu za kimataifa, haswa kutoka Irani.
Kwa hiyo nilitaka kuonana naye ili nijifunze kuhusu kazi zake, na nilipokutana naye na kufahamu kwamba alikuwa anatayarisha filamu kumhusu Mtume (SAW), nilifurahi sana, na niliona kuwa ni heshima kubwa kushirikiana naye.
IQNA: Ulichukuliaje kazi ya kutunga muziki wa filamu yenye umuhimu mkubwa wa kihistoria na kidini?
Rahman: Nilikuwa nikifuatilia kidogo muziki wa Kiarabu. Na wakati huo huo, nia ya Majidi ilikuwa kutayarisha filamu kwa watu wote duniani , sio tu kwa Iran, Saudi Arabia, au India; ni kwa ulimwengu kwa kila mtu kuiona. Kama alivyosema, kuna filamu nyingi sana zilizotengenezwa juu ya Nabii Isa (AS) lakini The Messenger ndio iliyokuwa filamu pekee ya Mtume Muhammad (SAW).
IQNA: Je, ulikumbana na changamoto yoyote wakati wa kufanya kazi kwenye mradi huu?
Rahman: Changamoto pekee ilikuwa kwamba Majidi hazungumzi Kiingereza. Anazungumza tu lugha ya filamu na sanaa. Kwa hiyo tulikuwa tukifanya kazi kwa njia tofauti sana. Kwa hivyo tulichukua muda ili tuwe na mtazamo mmoja wa kifikra kuhusu muziki. Kisha siku moja tukiwa Munich nilimpigia miziki mingi tofauti na kisha nikaelewa alichokuwa akitaka.
Ninajua kwamba nia yake ilikuwa nzuri sana; alitaka kueneza ujumbe wa amani na hekima ya Mtume Muhammad (SAW) kwa ulimwengu.
IQNA: Je uliiona filamu kwanza kabla ya kuitegenezea muziki?.
Rahman: Niliwahi kushuhudia sehemu ya filamu hiyo ikitegenezwa. Nilikuwa katika medani ya kutegeneza filamu hiyo sikku kadhaa. Kwa hivyo nilihisi nguvu na kile walichokuwa wakijaribu kufanya..
IQNA: Je, kulikuwa na mvuto wowote maalum wa muziki au mila ulizotegemea katika kuunda muziki huo wa filamu?
Rahman: Kimsingi ni muziki wa okestra yenye vipengele vya Kiarabu ndani yake. Baadhi miziki ni kama ile ya kwaya, kama wakati ule kijiji ambacho samaki wanakuja kutoka baharini, na wazo la sehemu hiyo lilikuwa ni kuonyesha muujiza uliotokea.
Majidi alikuwa na mambo mengi tofauti ambayo alitamani muziki utumike.
IQNA: Umetaja kwaya; Nilikuwa nikijiuliza ni nini mada kuu na msingi wa kwaya katika filamu hii.
Rahman: Katika kwaya kulikuwa na Salawat yaani kumsalia Mtume Muhammad (SAW) kwa hivyo kwa sababu katika muziki wa filamu hiyo tulihitaji kufikisha ujumbe na hivyo Salawat ilikuwa njia bora zaidi kwnai ni filamu ya Mtume (SAW).
IQNA: Kwa kuwa ni takriban muongo mmoja tangu kutolewa kwa filamu hiyo, unatathmini vipi mafanikio ya filamu yenyewe na muziki wake?
Rahman: Filamu kama inaibua hisia nyingi. Nia ni safi sana, na watengenezaji wanataka ujumbe uwafikie watu wengi zaidi ili kuunda daraja, walimwengu wamjue zaidi Mtume wetu, utamaduni, ubinadamu, upendo wa kina.
Lakini kwa bahati mbaya, kama kawaida, kuna mgawanyiko mwingi ulimwenguni. Wakati filimau ilipowekwa kwenye YouTube kwa Kiurdu na chaneli zingine nyingi, baadhi ya watu walishtuka; watu wengine walliipinga ni kudai si jambo sahihi.
Lakini nadhani jambo lililofanywa kwa nia njema huwa linajitokeza, na sasa unaweza kuona kwamba watu wanalitazama na wanaipenda.
Nilikuwa nimetabiri kwamba katika nusu ya miaka kumi itawavutia wengi zaidi kwa sababu watu wataiangalia kwa mtazamo mpana na wa kimantiki zaidi.
IQNA: Ni ujumbe gani mkuu au hisia ulijaribu kuwasilisha katika muziki wa filamu hii?
Rahman: Nadhani kwa ujumla yote ni kuhusu mapenzi. Na ukiangalia kila wimbo, kuna upendo katika idadi ndogo na kubwa. Na Mtume Muhammad (SAW) anahusu mapenzi. Na kwa hivyo kila sehemu ya muziki, isipokuwa sehemu ya vita dhidi ya mapagani.
IQNA: Kwa vile wewe pia ni mtaalamu wa mtindo wa Qawwali, unachukuliaje vipengele vya kiroho na kihisia vya kuigiza nyimbo zilizowekwa kwa ajili ya Mtume Muhammad (SAW)? Ni hisia gani unazopata zaidi wakati wa kuziimba?
Rahman: Nafikiri binafsi ninachohisi ni kama kioo cha vioo elfu moja. Unaona uso mmoja na kuangazia nuru elfu moja au hata zaidi isiyo na kikomo. Kwa hivyo chochote kinachotolewa kwa Mtume, Salawat, Durood Sharif, Fatiha au kila kitu kinaakisi kwako tu na watu walio karibu nawe. Siku zote ni kama baraka kukaa na kuimba qawwali. Na ni “Ibada” kwangu; kama vile unapotembea unasema Salawat au umekaa kwenye gari unasema Salawat, kuimba nyimbo za Mtume (SAW) ni Ibada kwetu.
Mahojiano yameandaliwa na Mohammad Ali Haqshenas