IQNA

Rais wa Iran

Inawezekana kuimarisha umoja na amani kimataifa kwa urafiki wa mataifa

23:39 - February 11, 2025
Habari ID: 3480199
IQNA-Rais katika sherehe ya ufunguzi wa Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Utalii ya Tehran alisema: Kuimarisha umoja, mshikamano, na amani ya kimataifa miongoni mwa mataifa ni jambo linalowezekana kupitia maingiliano na urafiki.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la IQNA; sherehe ya ufunguzi wa Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Utalii ya Tehran ilifanyika asubuhi ya leo, Jumanne, ikihudhuriwa na Masoud Pezeshkian; Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyyed Reza Salehi Amiri; Waziri wa Urithi wa Utamaduni, Utalii na Sanaa za Mikono na baadhi ya maafisa wa ndani, mabalozi na wageni wa nje katika eneo la maonyesho ya kudumu ya kimataifa ya Tehran.

Rais Pezeshkian katika sherehe hii alisisitiza umoja wa kitaifa na alinukuu aya ya Qur'ani inayosema: “Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani. “ (Al Hajj: 46)

Akifafanua alisema: “Ukweli ni kwamba macho hayawi kipofu, bali mioyo iliyo katika vifua vyenu ndiyo inayokosa kuona. Kusafiri na kushuhudia yaliyomo husababisha ukuaji, uzoefu, ustawi, umoja, na mshikamano miongoni mwa wanadamu.

Rais aliongeza: Maonyesho na mikutano ya kitamaduni huandaliwa kwa lengo hili ili uzoefu na mafanikio ya wanadamu yaonyeshwe na waweze kufahamiana.

Alifafanua kwa kuitaja aya nyingine ya Qur’ani Tukufu inayosema: Tembeeni katika ardhi, kisha muone ulikuwaje mwisho wa wa wale waliokadhibisha…

Akifafanua amesema wale wanaoona na kujifunza, upeo wa mawazo yao huwa mpana na wanapata uelewa bora wa dunia. Mbali na faida za kiuchumi za utalii, safari na ziara za jamii nyingine zinaweza kusaidia maendeleo ya mwanadamu katika nyanja zote.

Kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa ni kuanzisha amani na usalama wa kidunia na lengo hili linaweza kufikiwa kupitia mawasiliano, amani, urafiki na kuheshimiana, si kwa vita, mauaji, ubaguzi na uvamizi.

Rais Pezeshkian alisisitiza: Tunapaswa kuunda mazingira ambapo mataifa yote yanaishi pamoja. Tukisafiri kwenda nchi nyingine na kujifunza tamaduni na watu wao, mawazo ya awali na mitazamo potofu huondoka.

Alisema: Tuna uhusiano wa kirafiki na wa kindugu na majirani zetu na tunataka amani na utulivu na mataifa yote. Kila mtu anayekuja Iran ni mgeni wetu mpendwa na tuna uhusiano na nchi zote jirani na urafiki na undugu huu utaendelea kudumu.

Maonyesho haya ya awamu ya 18 yatafanyika kuanzia tarehe 11-15 Feruari ambapo nchi 14 ikiwemo Uturuki, Qatar, Malaysia, Thailand, Urusi, Uzbekistan, Tajikistan, Indonesia, Madagascar na UAE zina mabanda kwenye maonyesho.

Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Utalii ya Tehran yalianza na mtazamo na kauli mbiu "Amani ya Makabila ya Iran na Umoja wa Kitaifa".

4265465

captcha