IQNA

Mtazamo

Fahamu Sababu za Kutojibiwa Dua

1:35 - March 28, 2025
Habari ID: 3480450
IQNA – Mwanazuoni mwandamizi wa Kiislamu anachambua baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha dua tunazomuomba Mwenyezi Mungu kutokujibiwa. 

Akizungumza na IQNA, Ayatullah Mohammad Andalib Hamedani, mwanazuoni mwandamizi kutoka Chuo cha Kiislamu (Hauzah) katika mji mtakatifu wa Qom, ameangazia sababu saba kuu zinazoweza kupelekea dua kutozaa matokeo yaliyokusudiwa. 

Ayatullah Hamedani amesisitiza kwamba, ingawa mwenye kuomba dua anatarajia majibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hakuna uhakika kwamba dua hizo zitajibiwa. Akifafanua amesema, "Ili dua zijibiwe, masharti fulani lazima yatimizwe, na vikwazo vya kujibiwa viondolewe." 

Amesema kwamba miongoni mwa masharti hayo ni nia ya dhati ya mwenye kuomba na kutokuwepo kwa malalamiko yasiyotatuliwa kati ya muombaji na wengine. Halikadhalika, amebaini kuwa kuzuia au kudhulumu haki za wengine, iwe za kifedha au zinazohusu heshima, kunaweza kuzuia kukubaliwa kwa dua. 

Mwanazuoni huyo amesisitiza pia umuhimu wa kuwajibika kibinafsi katika hali ngumu. "Wakati mwingine tunakabiliana na changamoto kutokana na makosa yetu wenyewe," alielezea. 

Maamuzi mabaya ya kifedha au ukosefu wa mashauriano yanaweza kusababisha hasara ambazo dua peke yake haziwezi kurekebisha. Katika hali kama hizo, watu wanashauriwa kuunganisha dua na hatua za busara pamoja na marekebisho, alisema. 

Ayatullah Hamedani pia alizungumzia changamoto za maisha, akisisitiza kwamba hata manabii walikumbana na dhiki. Alieleza kwamba matatizo mara nyingi ni mitihani ya kimungu, na akawahimiza watu kutafuta msaada wa Mwenyezi Mungu wa kuvumilia magumu badala ya kutarajia maisha bila matatizo. 

“Dua inapaswa kuambatana na juhudi za bidii,” alibainisha mwanazuoni huyo. Ingawa miujiza ipo, kanuni kuu ni kwamba jitihada za binadamu ni muhimu pamoja na maombi ya kiroho. Kuomba riziki au uponyaji bila kufanya juhudi za kiutendaji ni kinyume na hekima ya Mungu, alisema. 

Sababu nyingine inayoweza kufanya dua kuonekana kutokujibiwa ni kipengele cha muda wa kimungu. "Huenda tukakosa uvumilivu wa kusubiri muda mwafaka na mazingira sahihi kwa dua zetu kujibiwa," alisema Ayatullah Hamedani, akiongeza kwamba imani katika hekima ya Mwenyezi Mungu ni muhimu. 

Ayatullah Hamedani pia amesisitiza umuhimu wa dua yenyewe. Mbali na kutafuta matokeo fulani, dua ni aina ya ibada inayomkurubisha mja kwa Mwenyezi Mungu, alieleza mwanazuoni huyo. 

Alitoa mfano wa Ahl al-Bayt (AS) ambao walihusika katika dua ndefu bila kutarajia majibu ya haraka. 

Mwisho, mwanazuoni huyo alibainisha kwamba thawabu za dua si za manufaa ya kidunia pekee. “Maisha ya kweli yako Akhera, na thawabu za dua zetu zinaweza kujidhihirisha huko,” alihitimisha, akinukuu aya ya 64 ya Surah Al-Ankabut: “Na haya maisha ya dunia si chochote ila pumbao na mchezo, lakini nyumba ya Akhera ndiyo Maisha (ya kweli); laiti wangalijua!”

3492514

Kishikizo: dua
captcha