IQNA

Israel Yaharibu Turathi za Kiislamu chini ya Msikiti wa Al-Aqsa

12:59 - September 01, 2025
Habari ID: 3481168
IQNA – Uongozi wa Palestina wa Jimbo la al-Quds umetangaza kuwa Israel inafanya uchimbaji haramu chini ya Msikiti wa Al-Aqsa ulioko Mashariki mwa al-Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, na kusababisha uharibifu wa athari za Kiislamu.

Katika tamko lililotolewa Jumapili, ofisi ya gavana ilisema kwamba video zilizovuja zinaonyesha majeshi ya Israel yakifanya uchimbaji wa chini ya ardhi katika eneo hili tukufu la Kiislamu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa uchimbaji huo unaharibu mabaki ya zama za Umawiyyin, ambayo ni ushahidi hai na wa wazi juu ya umiliki halali wa Waislamu katika eneo hilo.

Iliongeza kuwa hatua hizo za Israel zinakusudia kufuta utambulisho wa kihistoria wa Al-Aqsa na kubadilisha ukweli kwa manufaa ya dai la uongo la “Hekalu la Kale (Temple Mount)”.

Kwa mujibu wa uwakilishi huo, kazi hizo zinafanywa bila uwazi wowote na bila usimamizi wa kimataifa, na zinaweza kudhoofisha misingi ya kimuundo ya msikiti.

Maafisa wa Palestina walisema juhudi hizi ni sehemu ya njama pana za kuweka hali mpya ardhini ili kuendeleza mpango wa Kiyahudi wa kugeuza sura ya mji wa al-Quds.

Waliitaka jumuiya ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, na UNESCO kuingilia mara moja ili kukomesha uvunjaji huu na kuishitaki dola ya uvamizi.

Wapalestina kwa muda mrefu wamekuwa wakiripoti kuhusu uchanjaji wa handaki chini ya Al-Aqsa unaofanywa na Israel, kama sehemu ya mkakati wa kubadilisha sura ya kihistoria ya Mashariki mwa al-Quds.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Baraza la Waqf la Quds  linaloendeshwa na Jordan ndilo lenye mamlaka pekee juu ya mambo yote ya Msikiti wa Al-Aqsa.

Israel imekuwa ikidhibiti Mashariki mwa al-Quds tangu kuivamia katika Vita vya Waarabu na Israel vya mwaka 1967, na kisha ikaitwaa rasmi mwaka 1980 – hatua ambayo haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

 

3494440

captcha