IQNA

Mkuu wa ACECR: Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani kwa Wanafunzi Waislamu yadhihirisha umuhimu wa Diplomasi ya Qur’ani:

8:31 - August 17, 2025
Habari ID: 3481096
IQNA – Kiongozi wa Akademia ya Iran ya Elimu, Utamaduni na Utafiti (ACECR) amesema kwamba programu kama Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani kwa Wanafunzi Waislamu huchangia katika elimu ya kizazi kipya na kuimarisha diplomasia ya kitamaduni kupitia Qur’ani Tukufu.

Ali Montazeri alieleza jambo hilo wakati wa ziara ya Fatemeh Mohajerani, msemaji wa Serikali ya Iran, katika Shirika la Habari la Kimataifa la Qur’ani (IQNA) siku ya Jumamosi.

Alibainisha kwamba toleo la 7 la Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani kwa Wanafunzi Waislamu, ambalo kwa sasa lipo katika mwaka wake wa saba, linashirikisha kazi za wanafunzi Waislamu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Alisema mashindano hayo yameanza kwa awamu ya awali na kazi zilizopokelewa zinaendelea kuhakikiwa.

Ushiriki wa wanafunzi kutoka nchi 45 katika tukio hili unaonyesha umuhimu na thamani ya diplomasia inayotumia Qur’ani Tukufu na nafasi ya wanafunzi katika kuendeleza tamaduni ya Qur’ani, alisisitiza.

Jumuiya ya Qur’ani ya  Wanafunzi Waislamu Iran, inayooshirikiana na ACECR, imeandaa mashindano haya tangu mwaka 2006 kwa lengo la kukuza umoja na ushirikiano miongoni mwa wanafunzi wa dunia ya Kiislamu na kuinua kiwango cha shughuli za Qur’ani.

Tukio la mwaka huu linafuata matoleo sita yaliyofanikiwa ya mashindano haya, ambayo yalihudumia washiriki kutoka zaidi ya nchi 85 na kuwa na athari kubwa katika ushirikiano wa kitamaduni na Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu.

Toleo la 6 lilifanyika katika mji mtukufu wa Mashhad, kaskazini-mashariki mwa Iran, mnamo Aprili 2018.

Vilevile, katika mazungumzo yake wakati wa ziara ya Jumamosi katika ofisi za IQNA na msemaji wa Serikali, Montazeri alirejelea mashindano ya Qur’ani kwa wanafunzi nchini Iran na kusema kwamba yameandaliwa kwa heshima na utukufu wa kipekee.

Mashindano haya, mbali na kukuza vipaji vya vijana, yameweka fursa muhimu za diplomasia ya kitamaduni na kuendeleza Qur’ani Tukufu, alieleza.

3494276

captcha