Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi (SPA), washiriki wa Mashindano ya 45 ya Kimataifa ya Kuhifadhi, Kusoma na Kufasiri Qur’ani Tukufu walitembelea misikiti kadhaa ya kihistoria na maeneo ya kale mjini Madina.
Wizara ya Masuala ya Kiislamu imeeleza kuwa matembezi hayo yalikuwa sehemu ya programu ya kitamaduni iliyoandaliwa kwa ajili ya washiriki wa mashindano hayo ya mwaka huu. Programu ilianza kwa ziara katika Mlima Uhud, makaburi ya mashahidi wa Uhud, na Mlima Rumaah, ambapo washiriki walipatiwa maelezo kuhusu umuhimu wa kihistoria na kidini wa maeneo hayo.
Baadaye, walitembelea Msikiti wa Quba, unaotambuliwa kuwa msikiti wa kwanza kujengwa katika Uislamu, ambapo walipata taufiki kwa kuswali hapo. Kisha walielekea katika Msikiti wa Mtume (Al-Masjid an-Nabawi) na kuswali katika Rawdah al-Sharifah.
Raundi ya mwisho ya mashindano hayo ilihitimishwa Alhamisi katika Msikiti Mtakatifu wa Makkah, baada ya siku sita mfululizo za mashindano yaliyofanyika asubuhi na alasiri.
Toleo la mwaka huu liliwakutanisha washiriki 179 kutoka nchi 128, wakishindana katika makundi matano, huku zawadi zenye jumla ya riyali milioni 4 za Kisaudi zikitolewa.
Waandaaji walisema tukio hili linakusudia kukuza thamani za wastani na uvumilivu, sambamba na kuimarisha uhusiano wa Waislamu na Qur’ani Tukufu. Washindi watatangazwa na kutunukiwa zawadi katika sherehe ya kufunga itakayofanyika wiki hii ndani ya Msikiti Mtakatifu wa Makkah.
3494309