Zaidi ya misikiti 1,600 katika jamhuri hiyo inashiriki katika kuandaa programu hizo, ambazo zilianza siku ya Ijumaa.
Kila mwaka, Waislamu wa Tatarstan hujawa na hali ya kiroho katika mwezi wa Rabi al-Awwal, mwezi ambao ndani yake kuna siku ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (SAW), inayojulikana kama Milad -un-Nabi.
Kwa mwaka huu, Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu imepanga sherehe mbalimbali za kidini, vipindi vya elimu, na shughuli za kijamii katika misikiti zaidi ya 1,600 na maeneo 48, ikijumuisha semina za kielimu, makongamano, shughuli za kitamaduni na kisanii, mashindano, na michezo.
Matukio ya kwanza makubwa yalianza Ijumaa, Agosti 29, katika mji mkuu wa Tatarstan, Kazan, kwa sherehe ya hadhara katika uwanja uliopewa jina la mwanachuoni mkubwa wa Kitatar, Shahabuddin Marjani, ulioko katika Mtaa wa Kale wa Kitatar.
Tamasha hilo limevutia umati mkubwa kutoka jamii ya Kitatar na Waislamu wanaoishi katika eneo hilo, kwa kuwa limejumuisha vipindi mbalimbali vinavyochanganya mawaidha ya kidini na vipengele vya kitamaduni na kisanii vilivyo na maadili.
Aidha, mnamo Septemba 4, Msikiti Mweupe wa mji wa kihistoria wa Bulgar utakuwa mwenyeji wa tukio kuu la kuadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad (SAW).
Erik Arslanov, mkuu wa idara hiyo, amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kazan kuwa programu za mwaka huu zinafanyika ndani ya muktadha wa maadhimisho ya miaka 1,500 tangu kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Tamasha la mwaka huu linawajumuisha wanazuoni wa Kiislamu na wasomaji wa Qur’ani Tukufu, na litajumuisha maigizo yanayochukua msukumo kutoka maisha ya Mtume (SAW), nyimbo za Kiislamu au Nashid kwa lugha ya Kiarabu na Kirusi kutoka kwa kikundi cha Nashid al-Islam, mashindano maalum kwa watoto, na vipindi vya sanaa vinavyowasilishwa na wasanii wa Kitatar.
3494420