IQNA

Harakati za Qur'ani

Kijana mwenye ulemavu wa macho Misri ahifadhi Qur'ani kupitia redio

13:15 - August 23, 2022
Habari ID: 3475667
TEHRAN (IQNA) - Abdullah Mustafa, qarii wa Qur'ani Tukufu Misri mwenye ulemavu wa macho amehofadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu kwa kusikiliza kupitia redio na simu yake ya mkononi.

Abdullah Mustafa ni qarii wa Qur'ani Misri  ambaye anaweza kusoma kwa ustadi qiraa 10  na sasa ni mmoja wa wasomaji maarufu wa Misri mbali na kuwa  kocha wa maendeleo ya binadamu.

Yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Kitivo cha Wito cha Kiislamu cha Al-Azhar pia ni mtangazaji katika idhaa kadhaa za redio. Anasema: Mwanzoni, nilifikiri kwamba upofu ungekuwa kikwazo cha kufikia malengo yangu maishani, lakini niliweka mbali mawazo haya na kwa jitihada nimeweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu.

Abdullah ambaye ni miongoni mwa watu wa Bani Suif, alianza kuhifadhi Qur-aan akiwa na umri wa miaka 7 chini ya usimamizi wa Sheikh Abdullah Nadi, na akiwa na umri wa miaka 14, alihifadhi Qur'an kikamilifu.

Pia anasema kuhusu mbinu ya kuhifadhi Quran: Kwanza, nilianza kuhifadhi aya kwa kusikiliza sauti ya wasomaji wa Qur'ani kwenye redio, kisha nikaendelea na simu yangu ya mkononi.

Abdullah anaendelea kusema: Licha ya matatizo mengi niliyokuwa nayo, familia yangu, hususan baba, mama na kaka yangu, walinisaidia kwa njia hii na kuniandalia suhula nilizohitaji kwa juhudi kubwa.

Changamoto zinazomkabili Qarii mwenye ulemavu wa macho

Msomaji huyu mwenye ulemavu wa macho wa Misri anaichukulia moja ya changamoto kubwa inayomkabili kuwa ni kuwepo kwa mtazamo usiofaa na usio wa kweli wa uwezo wa vipofu katika jamii.

Kulingana naye, alikataliwa katika mahojiano mengi bila mtihani wowote kwa sababu tu alikuwa na ulemavu wa macho na kulikuwa na watu wengi waliomkatisha tamaa na kudhoofisha azma yake.

Katika ujumbe wake kwa jamii na viongozi wa Misri, Abdullah Mustafa amesema: "Vipofu na watu wenye mahitaji maalumu sio tu kuwa na uwezo wa kuhifadhi na kusoma Qur'ani, bali wana uwezo mwingi na maendeleo ya vipaji hivyo yanapaswa kuhimizwa hasa vijijini, kwa sababu maeneo haya yamejaa vipaji ambavyo havijagunduliwa.

Msomaji huyu wa Qur'ani , ambaye, mbali na kuhifadhi Qur'ani Tukufu, pia anafanya kazi kama mkufunzi wa maendeleo ya binadamu na mtangazaji wa redio, aliwataka vijana, hasa walemavu, kujitahidi kufikia malengo yao na kamwe wasikatishwe tamaa.

4079804

captcha