IQNA

Kampeni ya kuchangia Ibada ya Itikafu

18:44 - January 02, 2026
Habari ID: 3481754
IQNA-Kampeni ya ‘Nadhiri ya Itikafu’, ambapo watu wanachangia kugharamia ibada ya Itikafu misikitini imezinduliwa nchini Iran. Itikafu ni kujitenga kwa ajili ya ibada, na nadhiri ni ahadi ya kidini na jukumu la hiari.

Hujjatul-Islam Vahid Bolandi, Mkuu wa Masuala ya Kitamaduni na Kijamii katika Kituo cha Masuala ya Misikiti Iran, amesema kila msikiti hukusanya ada kutoka kwa washiriki wa ibada ya Itikafu. ‘Ndani ya mfumo wa kampeni ya Nadhiri ya Itikafu, tumewaomba watu kushiriki katika kugharamia wale wanaoshiriki Itikafu. Wale wenye uwezo wa kifedha lakini hawawezi kushiriki moja kwa moja katika ibada ya Itikafu wanaweza kushiriki kampeni hii kwa kutoa futari na daku kwa washiriki, na hivyo kupata thawabu za Itikafu,’ amesema.

Ameongeza kuwa ibada ya kiroho ya Itikafu mwaka huu itafanyika katika misikiti elfu moja katika mkoa wa Tehran. ‘Tumewaandalia maimamu wa misikiti inayofanya Itikafu kifurushi cha maudhui, ambacho kinajumuisha nyaraka za kitamaduni, dua na mawaidha,’ amesema.

Ameeleza pia kuwa mwaka huu jukwaa la kidijitali ‘Msikiti Wangu’ limeundwa ili kurekodi shughuli za misikiti katika uwanja wa Itikafu, na kwa kujisajili humo, misikiti huchagua aina ya Itikafu watakayoandaa. Bolandi amebainisha kuwa usajili wa wale wanaotaka kushiriki Itikafu ulianza mwanzoni mwa Rajab, na sehemu kubwa ya nafasi katika misikiti ya Tehran tayari imekamilika.

Mwaka jana, watu 110,000 walishiriki Itikafu katika misikiti ya mkoa wa Tehran, na takwimu za usajili wa mwaka huu zinaonyesha kuwa idadi ya washiriki itaongezeka. Mwaka jana, misikiti 800 ilikuwa na  ibada ya Itikafu.

Itikafu ni sunna ya Mtume Muhammad (SAW) na Ahlul-Bayt wake, na inachukuliwa kuwa ibada yenye malipo makubwa katika Uislamu. Ni ibada ya kiroho inayohusisha kukaa msikitini kwa siku kadhaa, kufunga na kusali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kwa kawaida hufanyika tarehe 13, 14 na 15 Rajab, mwezi wa saba katika kalenda ya Kiislamu, ambazo mwaka huu zinakadiriwa kuwa Januari 3, 4 na 5, 2026.

3495926

captcha