IQNA

Kuhitimishwa kwa Kozi ya Mtandao ya Sayansi ya Qur’ani Nchini Iraq

17:23 - May 24, 2026
Habari ID: 3482277
IQNA – Kozi ya kwanza ya mtandao kuhusu sayansi ya Qur’ani, iliyohudhuriwa na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali, imehitimishwa nchini Iraq.

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Kafeel, kozi hii iliandaliwa kwa juhudi za Kituo cha Mafunzo ya Hauza cha Mirath al-Anbiya (Urithi wa Manabii) kilichopo Najaf, ambacho kiko chini ya Idara ya Masuala ya Kiakili na Kitamaduni ya Haram Takatifu ya Hadhrat Abbas (AS).

Kituo hicho kiliandaa mafunzo haya kupitia mifumo ya mtandao, yakishirikisha wanafunzi 180 kutoka ndani na nje ya mipaka ya Iraq.

Sheikh Hussein Al-Turabi, Mkurugenzi wa kituo hicho, amesema kuwa kozi hiyo ilijumuisha uwasilishaji wa masomo na mijadala ya kina kuhusu sayansi za Qur’ani.

Al-Turabi alibainisha kuwa kituo hicho kilichagua kitabu cha “Darsa fi Uuluum al-Qur’ani” (Masomo ya Mbinu katika Sayansi ya Qur’ani) kilichoandikwa na Sayyid Riyad Al-Hakim kwa ajili ya kufundishia katika kozi hiyo kutokana na usahihi wake wa kisayansi. Wanafunzi walishiriki katika mijadala ya ana kwa ana (kwa njia ya mtandao) chini ya usimamizi wa maprofesa wabobezi, ili kuhakikisha kuwa wameelewa na wanaweza kutumia kikamilifu yale waliyofundishwa.

Alisisitiza kuwa malengo ya kozi hiyo yalikuwa ni kuendeleza ujuzi wa kisayansi wa watafiti na wanafunzi, kusambaza mbinu bora na sahihi za kielimu kwa ajili ya kuifafanua na kuielewa Qur’ani, pamoja na kuwaunganisha waumini na mitazamo ya wanazuoni na mafakihi wakubwa.

Kozi hiyo iligusia mada muhimu katika sayansi ya Qur’ani, ikiwemo historia ya Qur’ani, miujiza ya Qur’ani Tukufu, uhifadhi wa Qur’ani dhidi ya upotoshaji, na misingi ya tafsiri.

3497572

Kishikizo: iraq qurani tukufu najaf
captcha