IQNA

Miaka mitano baadaye, jamii ya London yaungana kuwakumbuka wanafamilia wa Kiislamu waliouawa kikatili katika shambulio la chuki

15:41 - June 07, 2026
Habari ID: 3482332
IQNA – Miaka mitano baada ya washiriki wanne wa familia moja ya Kiislamu kuuawa kwa kugongwa makusudi na gari katika kitendo ambacho jaji amekitaja kuwa ni cha kigaidi, wanajamii katika mji wa London, Ontario nchini Kanada, wamekusanyika kuwakumbuka wahanga hao na kusisitiza upya ahadi yao ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Bwana Salman Afzaal, mke wake Madiha Salman, binti yao Yumna na nyanya yake Talat, waliuawa mnamo Juni 6, 2021, baada ya mwanamume mmoja kuwagonga kwa lori lake walipokuwa wakitembea katika mtaa mmoja wa London, Ontario.

Mtoto wa kiume wa wanandoa hao, ambaye alikuwa na umri wa miaka tisa wakati huo, alijeruhiwa vibaya lakini alinusurika. Mshambuliaji huyo alipatikana na hatia ya mashtaka manne ya mauaji na shtaka moja la jaribio la mauaji mnamo mwaka 2023.

Jaji alitoa uamuzi kuwa mauaji hayo, yaliyofanywa na mtu aliyejitangaza kuwa ni mfuasi wa siasa kali za “utaifa wa kizungu” (white nationalist), yalikuwa ni kitendo cha kigaidi. Kesi hii iliweka historia nchini Kanada kama mara ya kwanza kwa sheria za ugaidi kutumiwa mbele ya baraza la wasuluhishi (jury) katika kesi ya mauaji ya daraja la kwanza.

Jaji aliongeza kuwa matokeo ya chuki “yanaweza kuwa ya maangamizi na mauti.” Alisema: “Kuna nyakati katika historia ya jamii ambazo huacha alama isiyofutika. Hii ilikuwa moja ya nyakati hizo kwa mji wa London.”

Aliongeza: “Tunawakumbuka si kwa kile walichopoteza tu, bali kwa jinsi kumbukumbu yao inavyoendelea kuhamasisha umoja, huruma, ujasiri na wajibu wa kusimama dhidi ya chuki katika aina zake zote.”

Maadhimisho haya ya miaka mitano yanakuja wakati shirika la kitaifa la Kiislamu likihimiza serikali ya Ottawa kutekeleza mapendekezo ya kushughulikia chuki dhidi ya Uislamu.

Akizungumza katika majengo ya Bunge siku ya Alhamisi, Khaled Al-Qazzaz, mkuu wa Baraza la Masuala ya Umma la Waislamu wa Canada (CMPAC), alisema shambulio dhidi ya familia ya Afzaal “lilifichua ukweli mchungu” wa chuki inayowakabili Waislamu kote nchini humo.

“Licha ya miaka mingi ya tafiti, mashauriano na ahadi za hadharani, Waislamu nchini Kanada wanaendelea kukumbana na ubaguzi, unyanyasaji, ghasia na kutendewa isivyo haki,” alisema Al-Qazzaz, ambaye kikundi chake kimetoa ripoti mpya inayohimiza serikali kupambana na chuki dhidi ya Waislamu.

Alisisitiza kuwa: “Islamophobia haijidhihirishi tu kupitia vitendo vya chuki vya mtu mmoja mmoja, bali pia kupitia mifumo mipana ya kijamii na kitaasisi ambayo inaendelea kudhuru na kuwanyima haki jamii za Kiislamu.”

Ripoti hiyo inaihimiza serikali ya shirikisho kutekeleza mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati za Bunge na Seneti ili kuongeza mafunzo ya kubaini na kuzuia ubaguzi. Pia, inatoa wito wa kutolewa kwa dola milioni 40 za kimarekani kwa ajili ya kulinda misikiti na shule za Kiislamu.

Aidha, kikundi hicho kinataka sera zitakazowawajibisha wamiliki wa mitandao ya kijamii kwa kueneza na kuchochea chuki mtandaoni, kikibainisha kuwa mauaji mengi ya halaiki nchini Canada yamefanywa na watu walioathiriwa na maudhui ya itikadi kali.

3497741

Habari zinazohusiana
captcha