
Siku ya Arafah ni tarehe ya tisa ya mwezi wa Dhul Hijjah katika kalenda ya Hijria, na ndiyo siku ambayo ibada kuu za Hija huanza rasmi.
Katika siku hiyo, mahujaji wote hukusanyika katika jangwa la Arafat (Arafah), wakimwomba Mwenyezi Mungu, kutubia na kumshukuru kwa kuwapa tawfiki ya kutekeleza ibada ya Hija.
Baada ya kuswali Sala ya Adhuhuri na Alasiri pamoja na kusoma dua katika vilima vya Jabal Rahmah, mahujaji huelekea Mash’ar al-Haram ili waweze kuwapo Mina siku ya Eid al-Adha.
Akizungumza na IQNA, mwanazuoni wa Hauza ya Qom, Hujjat al-Islam Amin Rassaf, alizungumzia kwa kina vipengele vya kiroho vya Siku ya Arafah, akiitaja siku hiyo kuwa ni hati ya kufikia uhuru wa kweli ambao, kupitia uhusiano wa kielimu na kiutambuzi baina ya mja na Muumba wake, huweka msingi wa kujitegemea kiroho dhidi ya nguvu za kidunia na kimada.
Alisema siku hiyo ni wakati wa “kuzaliwa upya kiroho” kwa mwanadamu, akifafanua kuwa Arafah ni kipindi ambacho elimu na maarifa hutoka katika mipaka ya fikra za kawaida na kuingia katika ulimwengu wa utambuzi wa moyoni na maono ya kiroho.
Akirejea historia ya Mitume Muhammad (SAW), alisisitiza kuwa Arafah imekuwa daima ni uwanja wa kukiri ukweli na kuinua kiwango cha ufahamu wa mwanadamu katika historia yote.
Katika daraja hilo la maarifa, alisema, mwanadamu hujenga upya uhusiano wake na ulimwengu wa uwepo na kupata uelewa mpya kuhusu uhusiano kati ya dunia ya maada na ulimwengu wa Kiungu.
Aidha, alieleza kuwa kuna uhusiano wa kimkakati na usiovunjika kati ya Arafah na Karbala, akisema kuwa bila ya kuelewa kwa kina Dua ya Arafah haiwezekani kupenya katika undani wa tukio la Ashura.
Kabla ya kuuawa shahidi, Imam Hussein (AS) aliweka wazi hakika ya tauhidi katika jangwa la Arafah kupitia lugha ya fikra na dua, amesema Hujjat al-Islam Rassaf.
Mwanazuoni huyo pia alizungumzia changamoto zinazoukabili ulimwengu wa kisasa, akiitaja Dua ya Arafah kuwa ni suluhisho la kuondokana na “mgogoro wa maana ya maisha”.
Aliongeza kuwa leo hii, kuliko wakati mwingine wowote, mwanadamu anakumbwa na upweke wa kudumu na hali ya utupu wa ndani, huku mafundisho ya Siku ya Arafah yakijaza pengo hilo la kiroho kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu ambaye uwepo Wake uko karibu na dhahiri kwa mja wake wakati wote.
/3497606