IQNA

Haram ya Imam Ali (AS) yatangaza utayari wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Ghadir

14:58 - May 26, 2026
Habari ID: 3482286
IQNA – Uongozi wa Haram Takatifu ya Imam Ali (AS) mjini Najaf, Iraq, umetangaza kuwa umekamilisha maandalizi yote ya kuendesha programu za Wiki ya Kimataifa ya Ghadir kwa mwaka 1447 Hijria.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ataba Alawiyya, Haram ya Imam Ali (AS) imekamilisha hatua zote za kiufundi, kiutawala na huduma maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Eid al-Ghadir ndani na nje ya Iraq.

Imeelezwa kuwa kutakuwa na programu pana na mbalimbali za kidini, kitamaduni, kimalezi, kiitikadi na katika vyombo vya habari zitakazolenga makundi tofauti ya jamii, ili kuadhimisha tukio hilo kwa namna inayostahiki hadhi na utukufu wake.

Aidha, idara zote pamoja na vikosi vya utekelezaji vya Ataba hiyo vitashiriki katika shughuli hizo kwa lengo la kuhakikisha siku hiyo inaadhimishwa kwa heshima kubwa.

Wissam Iskander, mkuu wa Kituo cha “Nazm” chini ya Kitengo cha Mipango Mkakati na Maendeleo cha Ataba hiyo, amesema Wiki ya Ghadir itashuhudia mkutano maalumu na waandishi wa habari kwa ajili ya kutangaza ratiba na maelezo ya programu za tukio hilo tukufu.

Alibainisha kuwa hapo awali uongozi huo uliandaa hafla katika Haram ya Imam Ali (AS), ambapo bendera zilizobarikiwa za Ghadir zilikabidhiwa kwa wawakilishi wa misafara, taasisi, mawakibu na mashirika ya kijamii kwa ajili ya kuandaa hafla za kupandisha bendera hizo katika maeneo yaliyotangazwa.

Iskander alisema pia katika hafla hiyo ilitangazwa kuwa zaidi ya bendera 150 za Ghadir zitapandishwa ndani na nje ya Iraq.

Kwa mujibu wake, programu za Wiki ya Ghadir zitajumuisha mashindano, vikao vya Qur’ani Tukufu, majlisi za kumbukumbu, hafla za kuwasaidia wahitaji pamoja na programu maalumu kwa watoto.

Naye Karrar al-Mousavi, mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma ya – Uongozi wa Haram Takatifu ya Imam Ali (AS), amesema katika mfumo wa programu za Wiki ya Eid al-Ghadir, zaidi ya bendera 150 zilizobarikiwa zitapandishwa katika hafla rasmi itakayoshirikisha ujumbe maalumu na wahudumu wa Haram Takatifu.

Alisema bendera za Ghadir zitapandishwa katika maeneo matakatifu na haram mbalimbali nchini Iraq, sambamba na maeneo 20 katika mikoa tofauti ya nchi hiyo kwa uratibu na mashirika, taasisi, mawakibu na makundi ya kijamii.

Al-Mousavi ameongeza kuwa bendera hizo pia zitapandishwa katika mikoa 20 ya Iran ambayo imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya Kizayuni na Marekani, pamoja na katika nchi nane za Ulaya, majimbo matano ya Marekani na maeneo mengine mbalimbali duniani.

Aidha amesema hafla ya kupandisha bendera hizo itaratibiwa kwa ushirikiano na vyombo vya habari vya kimataifa, huku wawakilishi rasmi na wa umma wakitarajiwa kushiriki.

Tukio la Ghadir au Eid al-Ghadir huadhimishwa kila mwaka na Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia kote duniani.

Ni miongoni mwa sikukuu muhimu na zenye furaha kubwa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia, huadhimishwa tarehe 18 Dhul Hijjah katika kalenda ya Hijria, ambayo mwaka huu itaangukia Alhamisi, Juni 4.

Kwa mujibu wa simulizi za Kiislamu, siku ya Ghadir ndiyo aliyomteua Imam Ali ibn Abi Talib (AS) kuwa khalifa na Imam baada yake, kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

3497605

captcha