
Ameashiria suala la taifa kubwa la Iran kuegemea kwenye ishara hizo hususan silaha ya “Allahu Akbar” tangu zama za harakati na hatimaye ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na vile vile zama za Vita vya Kujitetea Kutakatifu hadi Vita vya Pili na vya Tatu vya Kulazimishwa, na kushindwa adui kuilazimisha Iran ijisalimishe, na tukio la kimiujiza la kubaathiwa wananchi na kusisitiza: Mwaka huu, suala la kujibari na kujitenga mushirikina lina umuhimu maradufu.
Ujumbe kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Umma wa Kiislamu uliosomwa Jumanne asubuhi na Hujjatul Islam Walmuslimin Nawwab, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu na Msimamizi wa Mahujaji wa Iran katika Jangwa la Arafat ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu
Labbayka Allahumma labbayk, labbayka lā sharīka laka labbayk. Innal-ḥamda wan-ni‘mata laka wal-mulk.
Ee Mola wangu, nimeitika mwito Wako; huna mshirika wowote. Himdi zote, neema zote, ufalme na mamlaka yote ni Yako na yanatoka Kwako.
Msimu wa Hija wa mwaka huu umefika tena, na mahujaji wa Umma wa Kiislamu wamevaa ihramu ya utiifu na wanatamka Talbiya ili wahame kutoka maisha ya kidunia na ya kawaida kuelekea maisha ya Kimungu yenye fanaka; maisha ya Tauhidi yanayojengwa juu ya ibada kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, pamoja na kukataa, kujiepusha na kujitenga na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, fursa hii ya hijra au kuhamama si mahsusi kwa Mahujaji wa mwaka huu pekee. Inawahusu pia ndugu na dada wote Waislamu wa Iran na ulimwengu mzima , wale waliokwisha kuhiji katika miaka iliyopita, na pia wale ambao bado hawajapata tawfiki ya kutekeleza ibada ya Hija.
Sharti la hijra hii ni kufunga ihramu ya kudumu katika kumdhikiri Mwenyezi Mungu; kufanya tawafu ya kudumu kuzunguka mhimili wa haki; kufanya sa‘i ya daima kati ya vilele vya majukumu makubwa ya Kimungu; na ramy yaani kumpiga mawe Shetani muovu pamoja na sura zake za udanganyifu na wafuasi wake wote; kusimama kwa khushuu na dua; kuwalisha masikini na wahitaji; kutoa muhanga matamanio potovu ya nafsi na kuondoa uchafu wa ndani; na katika hali zote kuwa tayari kuitumikia haki na kuinua bendera ya kuitetea.
Ndivyo ilivyokuwa kwa taifa la Iran katika miqati ya Mapinduzi ya Kiislamu. Taifa hili liliitika mwito wa Kiibrahimu wa Imam Khomeini Mkubwa, likavua vazi la kunyenyekea kwa watawala wa kigeni, likavaa ihramu ya fanaka ya duniani na Akhera, na kwa kusema “Labbayk” na kukimbia kwa hima, likajitahidi kufanya tawafu kuzunguka mafundisho ya Uislamu safi wa Mtume Muhammad (SAW) na kujikaribisha kwenye nuru ya uadilifu wa kimataifa na Faqihi Mtawala.
Allahu Akbar, Allahu Akbar, lā ilāha illa Allah, wallahu Akbar, Allahu Akbar wa lillāhil-ḥamd.
Naam, Allahu Akbar. Kwa silaha hii ya “Allahu Akbar” ndipo taifa la Kiislamu la Iran liliposimama miaka 47 iliyopita, likaangusha utawala wa kitaghuti, kidikteta na tegemezi wa Pahlavi, likakata mikono ya Marekani yenye tamaa na yenye kiburi kutoka nchini humo, na kukomesha kabisa ushawishi wa Uzayuni.
Kwa silaha hiyo hiyo ya “Allahu Akbar” ndipo, baada ya uvamizi wa utawala wa Ba‘ath wa Saddam dhidi ya ardhi ya Iran, vijana mashujaa na wapiganiaji waliojitolea walipoandika historia ya miaka minane ya Kujihami Kutakatifu. Licha ya kuungwa mkono kwa utawala wa Ba‘ath na nguvu zote za Mashariki na Magharibi, waliuweka mahali pake, na wakaendelea kwa uthabiti mkubwa muqawama na mapambano dhidi ya mzingiro wa kiuchumi, majaribio ya kupindua serikali, vikwazo vya kidhalimu, na mashambulizi ya kisiasa, kiuchumi na kipropaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Allahu Akbar. Ni silaha hii hii ya “Allahu Akbar” iliyounganisha nyoyo za Umma wa Kiislamu na vijana Mujahidina wa mhimili wa muqawama kutoka Iran hadi Lebanon, Palestina, Iraq na Syria; kutoka Afrika na Yemen hadi Afghanistan, Pakistan na mataifa yote huru duniani, ili kamba hii madhubuti isimame kuitetea heshima ya Umma wa Kiislamu dhidi ya wavamizi Wazayuni, kusambaratisha njama Daesh (ISIS), kuanzisha Tufani al-Aqsa, na kufanya utawala dhaifu ya Kizayuni ushindwe kupumua.
Allahu Akbar. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkubwa kuliko maelezo yoyote. Kwa kutegemea silaha hii ya “Allahu Akbar”, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kuupiga kwa mapigo makali utawala wa Kizayuni katika vita vya pili vya kulazimishwa vya mwezi Juni 2025, na pia ikatoa kipigo kikubwa kwa Marekani, na kuwafanya maadui hao washindwe katika azma yao ya kuilazimisha Iran isalimu amri.
Na silaha ya “Allahu Akbar” ililipa taifa la Iran nguvu na uwezo mkubwa kiasi kwamba baada ya tukio la kusikitisha la kuuawa shahidi kwa Kiongozi Muadhamu aliyenawiri, mrithi mstahiki wa Mtume Muhammad )SAW), Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Husayni Khamenei , Mwenyezi Mungu Amrehemu, ambaye aliuawa kwa mikono ya waovu wa zama hizi, taifa hilo lilipata uhai mpya wa Kimungu na kwa uwepo wake katika kila uwanja uliokuwa ukihitajiwa, likayafanya macho ya dunia yabakie yakitazama fahari zake.
Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkubwa kuliko maelezo. Kwa silaha hii hii ya “Allahu Akbar”, wapiganaji mashujaa na vikosi vya kujitolea vya Iran ya Kiislamu, kwa kushirikiana na Mujahidin wa mhimili wa muqawama hususan Lebanon tukufu, walipata ushindi mkubwa dhidi ya majeshi mawili ya kigaidi, na yaliyojihami kwa idadi kubwa ya silaha, ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, katika vita vya tatu vya kulazimishwa. Kwa kutawakkul kwa Mola wao, walimvurumishia “Shetani Mkubwa” yaani Marekani na mnyama wake aliyepata mafunzo, yaani utawala Kizayuni, makombora na ndege zisizo na rubani nchi kavu angani na baharini, na wakayaona kwa macho yao ahadi za Mwenyezi Mungu za kuwasaidia wanaopigana katika njia Yake.
Na tena Allahu Akbar. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mkubwa kuliko maelezo yoyote, na majeshi Yake yanashinda nguvu zote. Kwa silaha hii hii ya “Allahu Akbar”, baada ya mwamko wa taifa la Iran na mhimili wa muqawama, mwamko wa Umma wa Kiislamu nao utatimia, na kujitenga na washirikina kutapanuka kutoka ibada ya kurusha mawe katika Hija hadi katika maisha ya binafsi, kijamii na kisiasa ya Waislamu kote duniani.
Umma wa Kiislamu na mataifa ya eneo hili yana uwezo mkubwa na maslahi ya pamoja ambayo yataunda nidhamu mpya na ramani ya baadaye ya eneo na dunia.
Mimi, kwa dhati na ikhlasi, ninazialika nchi na serikali zote za Kiislamu katika urafiki na kushirikiana katika mema, ili kwa pamoja tupige hatua kwa ajili ya maendeleo ya Umma wa Kiislamu na kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
Lililo wazi ni kwamba muda haurudi nyuma tena, na mataifa ya eneo hili hayatakuwa tena ngao za vituo vya kijeshi vya Marekani. Marekani haitakuwa tena na sehemu salama ya kufanya uovu na kuweka kambi zake za kijeshi katika eneo hili, na kila siku inazidi kupoteza nguvu zake za zamani. Aidha, utawala dhaifu na uvimbe wa saratani wa Kizayuni unakaribia mwisho wa umri wake wa kuchukiza, na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa kauli ya wazi na yenye maono ya Shahidi Kiongozi Muadhamu miaka kumi iliyopita, hautafikisha miaka 25 tangu wakati huo, In shaa Allah.
Kwa sababu hiyo, mwaka huu suala la kujitenga na washirikina lina umuhimu mkubwa zaidi. Kina na upana wa kujitenga na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni vimevuka mipaka ya ibada ya Hija pekee, na baada ya siku hizi tukufu, kauli mbiu ya “Mauti kwa Marekani” na “Mauti kwa Israel” itakuwa sauti ya kawaida ya Umma wa Kiislamu na wanyonge wa dunia, hususan vijana.
Mustakabali ni wa Umma wa Kiislamu na ustaarabu mpya wa Kiislamu, na kila mmoja wetu anaweza kutekeleza wajibu wake kwa kadiri ya hima, uwezo na jukumu lake katika kuifikia mustakabali huo. Mahujaji wa Iran katika Hija ya mwaka huu wana nafasi muhimu ya kuwaeleza ndugu zao Waislamu ushindi wa vita vya tatu vya kulazimishwa na kuwapa matumaini ya mustakabali wenye nuru.
Ninawaomba Mahujaji wote wapendwa kuzidisha dua kwa ajili ya kuharakishwa kudhihiri kwa Mwokozi wa wanadamu, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake; waombee umoja wa Umma wa Kiislamu, ukombozi wa Palestina na Msikiti wa al-Aqsa, kuondolewa matatizo makubwa ya Waislamu, na kufikiwa ushindi wa mwisho dhidi ya ubeberu wa kimataifa. Pia mnikumbuke katika dua zenu njema.
Ee Mola wetu! Mswalie Muhammad na Aali Muhammad, na uwajaalie Mahujaji na Umma mzima wa Kiislamu rehema na huruma Yako. Wape tawfiki ya Hija iliyokubaliwa, nyoyo zao uzitie nuru ya maarifa na basira, na uimarishe azma yao katika njia ya kuurekebisha Umma na kuufikia ushindi wa mwisho dhidi ya maadui wa Uislamu.
Ewe Mwenyezi Mungu! Ziteremshie neema na rehema zako kubwa roho safi za mashahidi wa njia ya Mwenyezi Mungu, haswa mashahidi wa mhimili wa Muqawama, wakiongozwa na, Kiongozi Muadhamu Shahidi, Mwenyezi Mungu ainue hadhi yake, na waongoze Mahujaji, wafanya-ibada na wanaofanya juhudi waliojumuishwa katika miongozo ya Kiongozi wa Umma. Liongoze taifa la Iran na Umma wa Kiislamu katika kuendeleza njia na lengo lake.
Ewe Mwenyezi Mungu, mteremshie baraka na salamu zako bora zaidi Imam Mahdi Anayesubiriwa, salamu na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na juu ya wazazi wake watoharifu. Na tujumuishe sisi sote na umma mzima wa Kiislamu katika dua zake za heri na zinazojibiwa. Ibariki dunia kwa ujio wake kwa sababu nyoyo zetu zimejaa yakini kutokana na hadi hiyo ya kweli. Kama unavyosema mwenyewe.
" Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu." (Qur'ani Tukufu 24:55)
Salamu, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya ndugu na dada zetu Waislamu.
Seyyed Mujtaba Hosseini Khamenei
Khordad 5, 1405
Dhul- Hijja 9, 1447
(May 26,2026)